1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macron na Merkel wataka mzozo Belarus kutatuliwa

21 Agosti 2020

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amependekeza kwamba Umoja wa Ulaya na Urusi zinaweza kusaidia kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Belarus.

https://p.dw.com/p/3hI7Z
Frankreich Bormes-les-Mimosas | Fort de Bregancon | Pressekonferenz Angela Merkel und Emmanuel Macron
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Pendekezo hilo ni sehemu ya kilichojitokeza katika mazungumzo kati ya Macron na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel yaliyofanyika siku ya Alhamisi huko kusini mwa Ufaransa. 

Viongozi hao wawili walizungumzia masuala mengi ikiwemo mgogoro wa kisiasa nchini Belarus pale walipokutana kwa saa kadhaa huko kusini mwa Ufaransa. Rais Macron na Kansela Merkel walizungumza pia na waandishi habari ambapo Macron alisema Umoja wa Ulaya unaweza kujaribu kuwa msuluhishi wa kumaliza mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na matokeo ya uchaguzi yaliyowakasirisha wananchi, yaliyompa ushindi Rais Alexender Lukashenko nchini Belarus.

Kiongozi huyo wa Ufaransa amesema wananchi wa Belarus wanapaswa kutafuta suluhisho, lakini pia akaongeza kusema Umoja wa Ulaya uko tayari kusaidia na kusisitiza kwamba Urusi inatakiwa kushirikishwa kwenye mazungumzo.

Russland Moskau Oppositionsführer Nawalny
Mwanasiasa wa upinzani wa Urusi, Alexei NavalnyPicha: Getty Images/AFP/K. Kudrayavtsev

Lakini pia ameionya Urusi dhidi ya kuchukua hatua yoyote ya kutumia nguvu kuingilia masuala ya ndani ya nchi jirani. Kwa upande mwingine Kansela Merkel amebainisha kwamba Rais Lukashenko hajachukua juhudi za kuzungumza na kiongozi yoyote wa Umoja wa Ulaya, licha ya kuendelea kukabiliwa na maandamano.

Ama kwa upande mwingine Ujerumani na Ufaransa zimelizungumzia pia suala la mwanasiasa wa upinzani na mkosoaji wa Rais Vladmir Putin, Alexei Navalny ambaye yuko mahututi hospitali, ambao wamesema nchi hizo zinajitolea kumpa huduma ya matibabu mwanasiasa huyo.

Kansela Merkel na Rais Macron wamesema wana wasiwasi mkubwa kwa kile kinachoendelea kwa mwanasiasa huyo, huku Macron akiongeza kusema kwamba Ufaransa iko tayari kumpa Navalny na timu yake huduma ya matibabu au hifadhi ya ukimbizi na ulinzi.

Kando na hilo Merkel na Macron pia walitowa mwito wa usalama na uthabiti katika eneo la mashariki mwa Bahari ya Mediterania kufuatia mivutano kati ya Ugiriki na Uturuki kuhusu haki ya uwezekano wa kuchimba mafuta na gesi asili. Walisisitiza juu ya kuheshimiwa kwa uhuru wa nchi za Umoja wa Ulaya. Lakini pia suala la mgogoro wa virusi vya corona liligusiwa ambapo Macron alisema nchi yake na Ujerumani sasa zina mkakati mpana wa pamoja unaojikita katika kuzuia, kupima na kutenga.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW