Macron na Putin kutafuta suluhisho la mzozo wa Ukraine
28 Januari 2022Mazungumzo hayo yanajiri baada ya mengine Alhamisi kati ya rais wa Marekani Joe Biden na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambapo Biden alimuahidi uungwaji mkono katika kukabiliana na Urusi.
Katika mazungumzo ya Biden na Zelensky, Biden alikariri utayari wa Marekani pamoja na washirika wake kutoa jibu kamilifu ikiwa Urusi itaivamia Ukraine.
Urusi: Majibu ya Marekani kuhusu Ukraine hayaridhishi
Hayo ni kulingana na taarifa kutoka Ikulu ya Biden White House, iliyoeleza pia kwamba Biden alisema Marekani inazingatia misaada zaidi ya kiuchumi kwa Ukraine lakini bila kutoa maelezo zaidi.
Kwa upande wake, Zelensky aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba walikuwa na mazungumzo mazuri ya simu na Biden, na kwamba walijadili juhudi za kidiplomasia kuondoa wasiwasi uliopo, na wamekubaliana kwa hatua za pamoja katika siku zijazo.
Wajumbe wa Ukraine na Urusi wakutana Paris
Juhudi zaidi za kidiplomasia zahimizwa
Biden amekuwa akiongoza juhudi za kutafuta mshikamano wa nchi za magharibi dhidi ya shinikizo za jeshi la Urusi kwa Ukraine, hatua ambayo imeighadhabisha Urusi.
Urusi imewarundika zaidi ya wanajeshi wake 100, 000 karibu na mpaka wake na Ukraine. Nchi za magharibi zinahofia huenda Urusi inataka kuivamia Ukraine. Madai ambayo Urusi imekanusha.
Biden atishia kumwekea Putin vikwazo binafsi
Wito wa kupatikana suluhisho la amani na kuepusha vita umekuwa ukitolewa na wakuu mbalimbali ulimwenguni mfano Waziri Makuu wa Slovakia Eduard Heger.
"Lengo letu ni kuondoa wasiwasi na kushiriki mazungumzo. Na tunapozungumzia baadhi ya madhara, tunafanya hivyo ili yasitokee. Kuhakikisha kuna suluhisho la amani dhidi ya mzozo na taharuki iliyoko,” amesema Heger.
Mazungumzo ya Macron na Putin yatarajiwa kutoa suluhisho
Kama sehemu ya juhudi za kidiplomasia za kusuluhisha mgogoro huo na kuondoa hofu kwamba Urusi inapanga kuivamia Ukraine, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wanatarajiwa kuzungumza Ijumaa kwa njia ya simu.
Macron anatizama mazungumzo kama nafasi ya kujua kwa yakini msimamo wa pande husika kuhusu hali ya sasa. Anatumai Putin atatoa maelezo kuhusu baadhi ya masuala.
Marekani yawaweka wanajeshi 8,500 tayari, mzozo wa Ukraine
Duru katika ikulu ya Macron zimesema rais huyo anataka kusisitiza kwa mara nyingine kwamba uvamizi wa Urusi nchini Ukraine utakuwa na madhara makubwa.
Mkuu wa kundi la walioshinda tuzo ya amani ya Nobel Beatrice Fihn ambaye pia anaongoza kampeni ya kuachana na matumizi ya silaha za nyuklia, ametahadharisha kwamba mzozo unaohusisha nchi zenye silaha za nyuklia ni hatari sana.
Fihn amesisitiza haja ya kumaliza mvutano kwa dharura, akitaja zana za nyuklia katika mpaka wa Urusi lakini pia kwingineko Ulaya, zinaweza kutumika endapo machafuko yatageuka vita.
Uingereza yatahadharisha kuhusu udukuzi kutoka Urusi
Katika tukio jingine, Uingereza imezitahadharisha biashara kubwakubwa kuchukua hatua za kuzuia uwezekano wa mashambulizi ya mitandao au udukuzi kutoka Urusi.
Wito huo wa tahadhari umetolewa na kituo cha usalama wa kitaifa kuhusu mitandao cha Uingereza.
Mkurugenzi wa operesheni wa kituo hicho Paul Chichester amesema wameweza kubaini matukio ya kutia mashaka ya kimtandao kutoka Urusi katika miaka ya hivi karibuni.
Mvutano kati ya Urusi na Ukraine ulianza mwaka 2014. Mkataba wa amani uliosimamiwa na Ufaransa na Ujerumani kusuluhisha utata bado umekwama.
(DPA,AFP,RTR)