Madaktari Sudan hatarini, huku mfumo wa afya ukiporomoka
18 Desemba 2024Madaktari nchini Sudan wanakabiliana na vita mnamo wakati huduma za afya zikiporomoka. Chama cha madaktari nchini humo kimesema asilimia 90 ya hospitali katika maeneo yenye machafuko, zimefungwa.
Milio ya risasi inasikika kwa mbali, ndege za kivita zinanguruma, na makombora yanarindima na kufanya ardhi kutetemeka.
Ndiyo hali nchini Sudan kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja na nusu tangu kuanza kwa vita vikali kati ya majenerali wawili mahasimu, Abdel Fattah al-Burhan anayeliongoza jeshi la taifa na Mohamed Daglo anayeongoza wanamgambo wa RSF.
Hayo yanapofanyika, wahudumu wa afya wanaotatanishwa na hali hiyo hawana chaguo mbadala, ila kuendelea kujaribu kutoa huduma kwa waathiriwa wa vita na wagonjwa wengine, lakini katika mazingira magumu.
Mohamed Moussa ni miongoni mwa madaktari hao na anasema masikio yake yamezoea kusikia milio ya risasi na makombora karibu na hospitali yake.
Unaweza kusoma pia: Jumuiya ya kimataifa haielewi athari za mgogoro wa Sudan?
Hospitali yake ya Al-Nao iliyoko eneo la Omdurman ni kati ya vituo vichache vya afya eneo hilo ambavyo bado vinatoa huduma kote Khartoum.
Machafuko hayo yamegeuza hospitali kuwa viwanja vya mapambano, hali inayowaweka wahudumu wa afya kama Moussa katika hatari kubwa.
Mfumo wa afya wasambaratika Sudan
Mfumo wa kiafya wa Sudan ambao hata kabla ya vita ulikuwa unajikokota kwa sasa umeporomoka.
Kulingana na picha za satelaiti zilizotathminiwa na maabara ya chuo kikuu cha Yale,(YEL) pamoja na chama cha madaktari wa Marekani na Sudan, miongoni mwa hospitali 87 zilizoko mji mkuu Khartoum, karibu nusu yazo ziliathiriwa na vita kati ya mwanzo wa vita hadi Agosti 26 mwaka huu.
Mnamo mwezi Oktoba, shirika la afya duniani (WHO) lilithibitisha mashambulizi 119 yaliyofanywa dhidi ya vituo vya afya nchini humo.
Unaweza kusoma pia: Wapiganaji wa RSF watuhumiwa kuhusika na uhalifu wa kivita Sudan
Chama cha kitaifa cha madaktari nchini Sudan kinakadiria kuwa katika maeneo ya machafuko nchini humo, asilimia 90 ya vituo vya afya vimefungwa kwa sababu ya vita, hivyo kuacha mamilioni ya watu bila huduma muhimu za afya.
Pande zote mbili katika vita hivyo vinaelekezewa lawama kushambulia zahanati, kliniki na hospitali.
Wahudumu wa afya 78 wameuawa tangu vita vilipoanza
Chama hicho cha madaktari kimesema jumla ya wahudumu wa afya 78 wameuawa tangu vita vilipoanza kwa kupigwa risasi au kutokana na mashambulizi ya makombora wakiwa kazini au wakiwa majumbani.
Sayed Mohammed, msemaji wa chama cha madaktari ameliambia shirika la Habari la AFP kwamba kila upande kwenye mzozo huo unaamini kwamba wahudumu wa afya wanashirikiana na upande pinzani, hivyo kusababisha mashambulizi dhidi yao.
Soma pia: MSF: Ugonjwa wa kipindupindu unaenea 'kwa kasi' Sudan Kusini
Mohammed amesisitiza kwamba hakuna uthibitisho wowote wa kushambulia wahudumu wa afya kwa sababu madaktari wanawatibu wagonjwa au waathiriwa bila ubaguzi.
Kyle McNally, mshauri wa kiutu wa shirika la madaktari wasiokuwa na mipaka MSF, amesema "ulinzi wa haki za rai na wagonjwa” umepuuzwa kabisa.
Mzozo wazorotesha utoaji huduma za afya
Ameliambia AFP kwamba muendelezo wa mashambulizi dhidi ya vituo vya afya umesababisha uharibifu wa vituo vyenyewe na hivyo umezorotesha pakubwa utoaji huduma.
Hivi karibuni, shambulizi la droni liliwaua watu tisa ndani ya hospitali kuu eneo la Darfur Kaskazini.
Kulingana na chama cha madaktari wa Sudan, wanamgambo wa RSF wamekuwa wakivamia hospitali ili kuwatibu wapiganaji wake ambao wamejeruhiwa vitani au kuwatafuta maadui. Chama hicho pia kimelishitumu jeshi la taifa kufanya mashambulizi ya angani dhidi ya vituo vya afya kote nchini humo.
Vita vya Sudan vimewaua maelfu ya watu na takriban watu milioni 12 wamelazimika kuyakimbia makaazi yao. Mashirika ya kimataifa yamesema machafuko hayo yamesababisha mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu ulimwenguni.
(AFPE)