1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafanikio na changamoto za demokrasia ya Tanzania

19 Septemba 2024

Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) 19.09.2024 kimetoa ripoti inayothmini hali ya demokrasia nchini Tanzania, ambayo inaonyesha mafanikio na changamoto za hali ya demokrasia katika taifa hilo la Afrika mashariki.

https://p.dw.com/p/4krcL
Internationaler Tag der Demokratie, Tansania
Siku ya Kimataifa ya Demokrasia na hali ya demokrasia Tanzania miongoni mwa wazungumzaji ni Joseph Warioba na Freeman Mbowe.Picha: Florence Majani/DW

Ripoti hiyo inatolewa wakati wadau walioshiriki mjadala wa ripoti hiyo, wakisisitiza maridhiano na amani kama njia kuu ya kuleta suluhu kwa yanayoendelea nchini ikiwamo utekaji, mauaji namadaiya kuminywa demokrasia kwa vyama vya upinzani.

Ripoti mpya ya  tathmini ya Hali ya Demokrasia nchini Tanzania imetolewa leo ikionyesha kuwepo changamoto na mafanikio kadhaa katika utekelezwaji wa misingi ya demokrasia. Miongoni mwa yaliyobainishwa katika ripoti hiyo ni kukua kwa uhuru wa maoni ikilinganishwa na kiwango kilichokuwepo 2015 hadi 2017.

Uhuru mkubwa wa jeshi la polisi katika huhuru wa kukutana nchini Tanzania

Maadhimisho ya siku ya demokrasia kwa Tanzania
Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Jaji Joseph Sinde WariobaPicha: Florence Majani/DW

Kadhalika ripoti hiyo imebaini kuwa jeshi la polisi limekuwa na mamlaka makubwa katika kuamua uhuru wa kukutana na kukusanyika hasa kwa vyama vya siasa. Mengine ni taarifa za upotoshaji na uzushi limeonekana kuwa kubwa na kuchagiza mgawanyiko na mtikisiko wa siasa, huku mamlaka makubwa aliyonayo msajili wa vyama vya siasa nchini vikitajwa kutengeneza misingi ya uvunjwaji wa demokrasia nchini.

Awali, kabla ya ripoti hii kutolewa, Mgeni rasmi katika mjadala huo, Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, alisisitiza maridhiano na majadiliano.

Uchaguzi wa mwaka 2019 na 2020 wafananishwa na mfumo wa chama kimoja

Kadhalika Jaji Warioba alisema, uchaguzi wa mwaka huu na wa mwaka ujao umebeba amani ya Tanzania huku akirejea uchaguzi wa mwaka 2019 na 2020, akiufananisha na mfumo wa chama kimoja cha siasa.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa TCD, Freeman Mbowe, ambaye pia niKiongozi Mkuu wa Chadema yeye alisema mwezi Septemba umekuwa mwezi mgumu kwa Chadema na kuongeza kuwa ni muhimu kusema ukweli ili kuliponya taifa, huku akirejea matukio ya mauaji na utekaji wa makada wa chadema, akisema bado hakuna demokrasia ya kweli nchini.

Hatua ya Chadema kusitisha maandamano ya nchi nzima

Siku ya Kidemokrasia
Mwenyekiti wa Chadema Freeman MbowePicha: Florence Majani/DW

Muda mfupi baada ya kumalizika kwa mjadala huo, Mbowe, alifanya mkutano na wanachama wa Chadema, na kutangaza kusitisha maandamano yaliyopangwa kufanyika nchi nzima, kuishinikzia serikali kuhusu matukio ya mauaji na utekaji.

Septemba 11 mwaka huu, 2024), Mbowe alisema nia ya maandamano hayo ni kudai uhai wa wanachama na viongozi mbalimbali wa chama hicho waliopotezwa. Wadau wengine katika mjadala huo, walisisitiza amani na mazungumzo, Mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, yeye pia alisistiza amani na majadiliano.

Soma zaidi:Polisi yamtia mbaroni kiongozi maarufu wa upinzani Tanzania

Kadhalika, ripoti ya TCD kuhusu hali ya demokrasia nchini, iliyojikita katika kuibua changamoto na mafanikio ya kidemokrasia kuanzia Septemba  2023 hadi Septemba 2024 ilibaini kuwa katika kipindi hicho yalifanyika marekebisho ya sheria, lakini bado katiba ikabaki ile ile, huku ripoti hiyo ikieleza kuna uhusiano mzuri kati ya Asasi za kiraia na serikali ingawa sheria bado si rafiki kwa CSO.

DW, Dar es Salaam.