1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya Katiba ya Romania yafuta uchaguzi wa rais

7 Desemba 2024

Mahakama ya Katiba ya Romania imeamuru kufutwa kwa duru ya kwanza ya uchaguzi, ambao mgombea wa mrengo mkali wa kulia alikuwa ameshinda, na imeagiza kuitishwa uchaguzi wa marudio.

https://p.dw.com/p/4nrgo
Romania - Calin Georgescu
Mgombea aliyeshinda duru ya kwanza ya uchaguzi nchini Romania, Calin Georgescu.Picha: Vadim Ghirda/dpa/picture alliance

Huku kukiwa na tuhuma wa uchaguzi huo kuingiliwa na Urusi, mahakama hiyo ilisema kwenye hukumu yake ya jana Ijumaa, kwamba ingelitolea ufafanuzi wa uamuzi wake baadaye.

Haijafahamika lini uchaguzi mpya utafanyika, ingawa uamuzi huu umetolewa zikiwa zimesalia siku mbili tu kabla ya duru ya pili ya uchaguzi iliyokuwa iwakutanishe Calin Georgescu aliyeshinda duru ya kwanza, na Elena Lasconi anayeelemea upande wa mataifa ya Magharibi.

Soma zaidi: Mgombea wa mrengo wa kulia aongoza uchaguzi wa Romania

Georgescu ameuokosoa uamuzi wa mahakama akiuita kuwa ni mapinduzi, lakini ameapa kuendelea na mapambano.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 62 anayeungwa mkono na Ikulu ya Kremlin, aliwashangaza wengi kwa ushindi wake kwenye uchaguzi wa Novemba 24, akiwa ameendesha kampeni zake zaidi kupitia mtandao wa TikTok.