Mahakama ya Kenya yazuia Ujenzi wa mtambo wa makaa ya mawe
26 Juni 2019Matangazo
Mradi huo wenye gharama ya dola bilioni mbili umepingwa vikali na wanaharakati wa ulinzi wa mazingira, na wenyeji wa kisiwa hicho.
Jaji Mohammed Balala ameubatilisha uamuzi wa awali ulioridhia kibali cha ujenzi kwa mwekezaji, Amu Power.
Balala amewataka wawekezaji kufanya tathmini mpya ya athari za kimazingira, ambazo mtambo huo unaweza kusababisha katika kisiwa cha Lamu kilicho katika Bahari ya Hindi, ambacho kimeorodheshwa na shirika la UNESCO miongoni mwa Turathi za dunia.
Kampuni ya Amu Power inazo siku thelathini za kukata rifaa. Mahakama pia imesema umma wa Kenya haukushauriwa ipasavyo kuhusu mradi huo wa umeme unaozalishwa kwa makaa ya mawe, ambao ungekuwa wa kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki.