Mahakama ya kimataifa ICC yamhukumu Bemba
18 Septemba 2018Matangazo
Mahakama ya kimataifa ya mjini The Hague, ICC, imemhukumu mwanasiasa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Jean-Pierre Bemba faini ya dola laki tatu na kifungo cha mwaka mmoja jela kwa kosa la kuvuruga ushahidi.
Hata hivyo, Bemba hatakwenda jela kutokana na muda ambao ameshautumikia kifungoni hapo awali. Mwanasiasa huyo alifutiwa mashtaka ya kutenda uhalifu wa kivita baada ya kukata rufani mnamo mwezi wa Juni, lakini alihukumiwa kwa mashtaka ya uzito wa chini ya kuvuruga ushahidi.
Hukumu hii ya leo inazizima kabisa jitihada za Bemba kugombea katika uchaguzi wa urais utakaofanyika mnamo mwezi Desemba katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambao tangu hapo alishazuiliwa na Tume ya Uchaguzi na Mahakama ya Katiba ya nchi yake.