1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makamanda wa jeshi wa Uturuki , wataka rais wake kuamini katika mtengano kati ya dini na serikali.

Sekione Kitojo13 Aprili 2007

Kiongozi wa taasisi yenye nguvu nchini Uturuki ya jeshi ametoa onyo kali kwa chama tawala cha AK siku ya Alhamis , akisema kuwa rais atakayeingia madarakani anapaswa kuwa muumini halisi wa mfumo wa nchi hiyo wa kutenganisha dini na serikali. Pia Jenerali huyo Yasar Buyukanit , ambaye anafahamika sana kwa mawazo yake kupenda matumizi ya nguvu za kijeshi , pia alitoa wito rasmi wa kuingilia kijeshi kaskazini mwa Iraq ili kupambana na waasi wa Kikurd kutoka Uturuki ambao wanajificha huko.

https://p.dw.com/p/CHGN

Matamshi yake hayo yanaonekana kusababisha hali ya wasi wasi kati ya viongozi wa juu wanaounga mkono hali ya mtengano kati ya dini na serikali, ikiwa ni pamoja na majenerali wa jeshi na majaji, na chama tawala cha AK, ambacho kina mizizi yake katika siasa za dini ya Kiislamu, kabla ya uchaguzi mwezi wa May.

Tunamatumaini kuwa rais ajaye atakuwa mtu ambaye kwa dhati kabisa anafungwa na maadili ya msingi hii ya umma, ikiwa ni kutenga dini na serikali, na sio mtu ambaye anasema tu lakini hatendi mambo hayo, Buyukanit ameuambia mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya jeshi.

Nina matumaini kuwa rais kama huyo atachaguliwa. Lakini uamuzi utabaki mikononi mwa bunge, ameongeza kusema katika mkutano huo , uliohudhuriwa na uongozi mziwa wa ngazi ya juu wa jeshi.

Katika mwezi May , bunge la Uturuki linatarajiwa kumchagua mrithi wa rais Ahmet Necdet Sezer, muumini mkubwa wa mfumo wa utengano baina ya dini na serikali ambaye amekuwa na uhusiano wa karibu na jeshi katika kipindi chake cha utawala cha miaka saba.

Wapendelea mtengano huo kati ya dini na serikali nchini Uturuki wana wasi wasi kuwa waziri mkuu Tayyip Erdogan , ambaye zamani alikuwa anaelemea zaidi katika masuala ya dini , anaweza kuchukua nafasi hiyo ya kazi ya juu kabisa na kuanza kukandamiza hali hiyo ya mtengano kati ya serikali na dini.

Msingi wa mtengano , utaifa na serikali yenye nguvu ni nguzo muhimu za jamhuri ya kisasa ya Uturuki.

Kusema kwamba rais ajaye hapaswi kutamka tu kukubali maadili hayo ni ujumbe ambao unampunguzia nguvu Tayyip Erdogan. Tunafahamu kuwa Buyukanit ametumia maelezo hayo akimlenga Erdogan, Cengiz Candar , mwandishi maarufu wa CCN nchini Uturuki amesema.

Ina maana kuwa tuna wasi wasi, lakini hotuba yake yote inaonyesha kuwa majeshi ya Uturuki hayataingilia kati hatua za kumchagua rais, amesema.

Erdogan hajasema iwapo atagombea lakini idadi kubwa ya wanachama wa AK wanasema kuwa wanataka yeye awe rais. Atakuwa rais wa kwanza wa Uturuki akiwa na mwelekeo wa dini ya Kiislamu zaidi.

Chama cha AK kinatarajiwa kumtaja mgombea wake Jumatano ijayo. Kwa kuwa chama hicho kina wingi mkubwa bungeni, na ni dhahiri basi mgombea wake atachukua wadhifa huo.

Erdogan , ambaye ni mwanasiasa maarufu sana miongoni mwa raia wa Uturuki ambaye amesimamia hatua za ukuaji mkubwa wa uchumi na kuanzishwa kwa mazungumzo ya uanachama, na umoja wa Ulaya , anakana kuwa ana ajenda za kidini.

Wakati mbinyo wa kisiasa umeongezeka kutoka kwa upinzani dhidi ya Erdogan , raia wamekuwa kimya. Lakini maandamano ya kuunga mkono mtengano kati ya serikali na dini siku ya Jumamosi katika mji mkuu Ankara yanatarajiwa kuonyesha kiwango cha upinzani dhidi ya Erdogan kuwa rais.

Masoko ya fedha pia hupata baridi kutokana na matamshi ya kisiasa kutoka katika jeshi, ambalo limeweza kuziondoa serikali nne katika miongo michache iliyopita, na hivi karibuni kabisa mwaka 1997 iliiondoa madarakani serikali ya waziri mkuu ambaye anadhaniwa kuwa ni Muislamu mno. Sarafu ya Lira imedhoofika hadi kufikia kiasi cha Lira 1.37 kwa dola moja ya Marekani kutokana na matamshi ya Buyukanit wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuwa anataka Uturuki ifanye shambulio la kijeshi dhidi ya waasi wa chama cha PKK wanaojificha nchini Iraq.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa wito wa kuwashambulia waasi wa PKK unaokuja baada ya kuzidi mashambulizi kati ya waasi na majeshi ya ulinzi, utailetea mbinyo zaidi serikali ya chama cha AK.