Makumi ya watu wauawa Gaza
15 Januari 2024Wizara ya afya katika Ukanda wa Gaza inayodhibitiwa na kundi la Hamas imesema karibu watu 60 wameuawa kufuatia mashambulizi makali ya Israel yaliyoripotiwa kwenye miji ya kusini mwa Gaza ya Khan Younis na Rafah, pamoja na viungani mwa mji wa Gaza katika eneo la kaskazini.
Wizara hiyo imesema kuwa hospitali mbili, shule ya wasichana na nyumba kadhaa vilishambuliwa. Jeshi la Israel halijazungumzia chochote juu ya taarifa hii.
Rais wa Marekani Joe Biden ametoa taarifa katika siku hii inayoadhimisha siku 100 za kuzuiliwa zaidi ya watu 130, wakiwemo Wamarekani 6, ambao bado wanashikiliwa mateka na Hamas huko Gaza.
Biden amesema amekuwa akiwafikiria kila siku mateka hao na familia zao, na kwamba timu yake ya usalama wa taifa na yeye mwenyewe wamekuwa wakifanya kazi bila kukoma ili waweze kuachiliwa huru.
Hata hivyo, Seneta wa chama cha Republican, Rick Scott amemkosoa Rais Biden kwa kuruhusu Wamarekani wasio na hatia, Waisraeli na watu wengine kukamilisha siku 100 kama mateka huko Gaza, huku akikosoa kile alichokiita "udhaifu usio na kifani wa Biden" kwa kutuma pesa za ushuru za Wamarekani kwa Mamlaka ya Palestina ambayo amesema inawafadhili na kuwasaidia magaidi wa Hamas."
Soma pia: Maandamano yaanza Israel kutaka mateka wakombolewe
Kundi la wapiganaji la Hamas limechapisha video ya mateka watatu wa Israel na kusema hatima yao itafahamika leo Jumatatu.
Miito kutoka China na Australia
China imetoa wito wa kufanyika mkutano wa kilele wa amani. Akizungumza nchini Misri mwishoni mwa wiki, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amehimiza "kuundwa kwa ratiba maalum kwa ajili ya utekelezaji wa 'suluhisho la serikali mbili' na harakati za kurejeshwa haraka mchakato wa mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina.
Soma pia:Umoja wa Mataifa: Hali Ukanda wa Gaza inatisha
Huko Australia katika mji wa Canberra watu wameandamana kuiunga mkono Palestina, Hash Tayeh, ni mmoja wa waandamanaji:
"Na maana ya haki, ni kukomesha mauaji kwenye pande zote mbili. Watoto hawastahili kufa, wawe ni Wapalestina, wawe ni Wayahudi, wawe Wakristo, Wabuddha, au wasio na imani yoyote ya dini. Watoto hawastahili kufa kabisa."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Australia Penny Wong ambaye ameanza ziara yake huko Israel, Jordania, Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu ametoa wito wa usitishwaji mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas.
(Vyanzo: Mashirika)