1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Boubacar Keita aliahidi kukomesha mapinduzi nchini Mali

19 Agosti 2020

Mwezi mmoja baada ya kuchaguliwa na kuwa rais wa Mali mnamo 2013, Ibrahim Boubacar Keita alitangaza kwamba siku za wanajeshi wenye nia ya kudhoofisha nguvu ya serikali zimefika mwisho wake.

https://p.dw.com/p/3hCYm
Mali I Ibrahim Boubacar Keita
Picha: Getty Images/AFP/P. Ekpei

Kiongozi huyo alisema hayo huku akitolea mfano kambi ya kijeshi ya Kati iliyo nje ya mji mkuu ambapo uasi wa mwaka uliopita ulisababisha kuondolewa madarakani rais wa wakati huo Amadou Toumani Toure. Miaka saba baadaye, Keita,mwenye umri wa miaka 75, amejikuta kwenye hatima ile ile iliyomkuta mtangulizi wake.

Boubackar Keita alipinduliwa siku ya Jumanne tarehe 18.08.2020 katika mapinduzi ya kijeshi ambayo uasi wake ilianzia kwenye kambi ya Kati. Katika masaa machache, risasi zilisikika hewani huku waasi hao wakiendesha magari kuelekea mjini, na hatimae wakamtia nguvuni rais Keita, na kumpeleka kwenye kambi ya Kati ambako alilazimishwa ajiuzulu na pia kulivunja bunge.

Licha ya ahadi kemkem juu ya kumaliza matatizo ambayo yalisababisha kung'olewa madarakani mtangulizi wake, matatizo ya usalama yanayosababishwa na makundi ya waasi wa kaskazini mwa Mali pamoja na maoni ya umma kwamba rushwa imekithiri ndio mambo hayo hayo yaliyosababisha kutenguliwa kwa rais Keita.

Mgogoro wa uchaguzi wa bunge uliofanyika mnamo mwezi Aprili na uchumi uliosambaratika vilizidisha hasira za raia wa Mali, hali ambayo iliwafanya maelfu ya watu kuandamana katika mitaa ya mjini Bamako katika wiki za hivi karibuni waliomtaka kiongozi huyo ajiuzulu.

Kanali-meja Ismael Wague,kiongozi wa wanajeshi waliomuasi rais Boubacar Keita
Kanali-meja Ismael Wague,kiongozi wa wanajeshi waliomuasi rais Boubacar KeitaPicha: picture-alliance/dpa/AP/Ortm TV

Keita, maarufu sana kwa kuitwa kutokana na herufi za kwanza za majina yake IBK, alishinda uchaguzi wa marudio miaka miwili iliyopita na serikali yake ya muungano ilikuwa na uungwaji mkono mklubwa bungeni.

Ibrahim Maiga, mtafiti wa nchini Mali kutoka kwenye Taasisi ya Masomo ya Usalama amessema rais Keita hakuweza kuelewa haraka hasira iliyokuwepo miongoni mwa jamii nzima. Maiga amesema kiongozi huyo hakuzisoma alama za nyakati kwamba kulikuwepo na mahitaji makubwa ya mabadiliko nchini humo.

Keita aliingia madarakani akiwa na sifa ya kuwa mtu aliyekuwa sio mwepesi kutingihswa kwa kuzingatia enzi alipokuwa waziri mkuu katika miaka ya 90 wakati alipochukua maamuzi magumu dhidi ya waliounga mkono na waandaaji wa mgomo wa vyama vya wafanyikazi. Lakini tangu mwanzo hakuweza kupata suluhisho la kuushughulikia mgogoro uliotishia usalama wa Mali kaskazini mwa nchi hiyo.

Vikosi vya Ufaransa viliingilia kati mnamo Januari 2013 na kuwarudisha nyuma wapiganaji wenye misimamo mikali wanaohusiana na kundi la kigadi al Qaeda ambao walitumia uasi wa kabila la Tuareg na wakafaulu kudhibiti theluthi mbili ya eneo la kaskazini mwa nchi.Serikali ya rais Keita ilikuwa inapambana kuwadhibiti wanamgambo wa Tuareg waliokuwa wanataka kujitenga.

Kukithiri kwa rushwa serikalini

Rais Boubacar Keita aliungwa mkono sana na jamii ya kimataifa, haswa kutoka kwa mkoloni wa Mali wa zamani Ufaransa, nchi ambayo ilimwaga pesa nyingi nchini humo pamoja na na askari. Lakini serikali Keita yake ilijikuta inakabiliwa na lawama na madai ya ulaghai kuhusiana na ununuzi wa ndege ya rais iliyogharimu dola milioni 40 na matumizi mabaya katika ununuzi wa vifaa vya jeshi hatua iliyosababisha Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kuchelewesha misaada kwa muda.

Ahmedou Ould-Abdallah, mwanadiplomasia wa Mauritania na Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Mataifa katika Afrika Magharibi amesema wakati ambapo kuna uwepo mkubwa wa jeshi la nje, fursa za ufisadi nazo huwa kubwa.

Mwanawe rais Keita bwana Karim Keita anakabiliwa na lawama za kuhusika na ufujaji fedha za umma kutokana na jinsi anavyoishi maisha ya juu na vyeo alivyonavyo ikiwa ni pamoja na kuwa mwenyekiti wa kamati za bunge za ulinzi na usalama.

Katika runinga mapema siku ya Jumatano, msemaji wa kundi lililomg'oa keita madarakani alikosoa nguvu za kisiasa na usimamizi wa mambo ya serikali zilizokuwa chini ya familia ya Keita.

Msemaji huyo wa umoja wa M5-RFP Nouhoum Togo alieleza kwamba, IBK, yaani Ibrahim Boubacar Keita hakutaka kuwasilikiza watu wake ndipo maandamano dhidi yake yalipoanza na yeye kwamba Ufaransa au jamii ya kimataifa itamuokoa.

Chanzo:/RTRE