Mizunguko ya MINUSMA yasitishwa na Mali
15 Julai 2022Wizara ya mambo ya nje ya Mali imesema katika taarifa kuwa mizunguko ya ujumbe wa MINUSMA inasitishwa, ikijumuisha ile ambayo tayari imepangwa. Hatua hiyo itadumu hadi mkutano ufanyike ili "kuwezesha uratibu na udhibiti" wa mzunguko wa vikosi hivyo. Hata hivyo tangazo hilo halikueleza sababu za hatua hiyo.
Hayo yanajiri siku nne baada ya Mali kuwakamata wanajeshi 49 wa Ivory Coast ambao baadaye iliwataja kama "mamluki" wenye nia ya kuipindua serikali inayoongozwa na jeshi la nchi hiyo.
Ivory Coast inadai wanajeshi hao ni wa vikosi vya Msaada wa Kitaifa (NSE), ambao utaratibu wa Umoja wa Mataifa unawaruhusu vikosi vya kulinda amani kutumia wasaidizi wa nje kwa majukumu kadhaa.
Kulingana na Ivory Coast, wanajeshi hao, ambao walikamatwa baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Bamako wakiwa katika ndege maalum, walijumuisha mzunguko wa nane chini ya mpango huo.
Taarifa ya Mali ya jana Alhamisi haikurejelea kukamatwa kwa raia hao wa Ivory Coast, wala haikutoa tarehe ya mazungumzo ya kujadili mizunguko ya MINUSMA.
Lakini iliuhakikishia ujumbe wa Umoja wa Mataifa kwamba Mali "itatumia kila njia ili kuweka mazingira bora ya kuondolewa kwa usitishwaji wa mzunguko huo, ambao wamesema ni hatua muhimu katika kuwezesha utekelezaji mzuri wa mamlaka ya MINUSMA.
Kwa upande wake, MINUSMA imesema katika taarifa yake fupi kuwa imezingatia uamuzi wa Mali lakini ikasisitiza kuwa iko tayari kushiriki haraka iwezekanavyo katika majadiliano, na kuongeza kuwa mzunguko huo una jukumu muhimu katika kudumisha ufanisi wa utendaji wa ujumbe wake pamoja na ari ya wafanyakazi wake.
Matokeo ya hatua hiyo kwa MINUSMA
Mtaalam wa Ujerumani Ulf Laessing ambaye anaongoza mpango wa eneo la Sahel wa Konrad Adenauer, anasema uamuzi huu lazima utakuwa na matokeo kwa askari wa Minusma:
"Ninaelewa kwamba raia wa Mali wanataka kuanzisha sheria mpya za mzunguko kama walivyofanya kwa safari za ndege za Minusma ambazo lazima kwanza ziidhinishwe na serikali ya Bamako. Kesi ya Ivory coast ni nyeti kwa sababu Abidjan inachukuliwa kuwa mshirika wa karibu wa koloni wa zamani, Ufaransa. Natumai pande zote zitakubaliana juu ya suluhu, la sivyo Minusma itapata ugumu wa kufanya kazi ipasavyo, na baadhi ya nchi zinaweza kusita linapokuja suala la kuendelea kutuma wanajeshi kushiriki katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali. »
MINUSMA ni Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kurejesha Utulivu nchini Mali, uliozinduliwa mwaka 2013 ili kusaidia mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani kukabiliana na vitendo vya umwagaji damu vya makundi yenye itikadi kali. Ni moja ya operesheni kubwa zaidi za kulinda amani za Umoja wa Mataifa, ikiwa na wanajeshi 12,200 na polisi 1,700 waliotumwa na baadhi ya nchi 50.
(AFP)