1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mali yatangaza kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine

5 Agosti 2024

Uamuzi huo ni baada ya Mali kuituhumu Ukraine kwa kuhusika katika mapigano kati ya jeshi lake na waasi wanaotaka kujitenga.

https://p.dw.com/p/4j7PB
Wapiganaji wa Vuguvugu la Ukombozi la Azawad wanaowania kujitenga na Mali.
Wapiganaji wa Vuguvugu la Ukombozi la Azawad wanaowania kujitenga na Mali.Picha: Souleymane Ag Anara/AFP/Getty Images

Msemaji wa serikali ya kijeshi ya Mali, Kanali Abdoulaye Maiga, alilaani matamshi ya msemaji wa shirika la ujasusi la kijeshi la Ukraine, Andriy Yusov, aliyekiri jukumu la nchi hiyo kuhusika katika mapigano yaliyosababisha vifo vya wanajeshi wa Mali na wapiganaji mamluki wa kundi binafsi la kijeshi la Urusi, Wagner katika mapambano ya mwishoni mwa mwezi Julai katika eneo la kaskazini ya Mali.

Mapigano makali ya siku tatu yalizuka karibu na mpaka kati ya Mali na Algeria tarehe 25 Julai katika kambi ya kijeshi ya Tinzaouatene.

Soma zaidi: Mali yasema inavunja uhusiano wa kidiplomasia na Ukraine

Waasi wanaotaka kujitenga wakiongozwa na Watuareg walisema waliwaua wapiganaji 84 wa kundi la Wagner na wanajeshi 47 wa Mali.

Waziri Mkuu wa Mali, Choguel Kokalla Maiga, alikiri kwamba jeshi la serikali lilishindwa vibaya katika vita vya Tinzaouatene.

Kanali Maiga amesema hatua ya Ukraine imekiuka mamlaka ya Mali na kwamba huo ni uingiliaji wa kigeni usiokubalika, ambao ni sawa na kuunga mkono ugaidi wa kimataifa.