Raia wa Niger washinikiza kuondoka kwa vikosi vya Marekani
22 Aprili 2024Hayo yanajiri wakati ujumbe kutoka Washington ukitarajiwa kuwasili nchini humo siku chache zijazo ili kupanga mikakati ya kujiondoa katika taifa hilo linalotawaliwa na jeshi.
Maandamano hayo yalishuhudiwa katika mji wa kaskazini mwa jangwa wa Agadez , kunakopatikana kituo cha anga cha Marekani, na yaliitishwa na kundi la vyama 24 vya kiraia ambavyo vimekuwa vikiinga mkono serikali ya kijeshi tangu mapinduzi ya mwaka jana.
Marekani iliafiki siku ya Ijumaa kuwaondoa wanajeshi wake zaidi ya 1,000 katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi ambako Marekani ilijenga kambi yake kubwa ya kijeshi yenye thamni ya dola milioni 100 ambayo pia ilikuwa ikitumiwa kurusha droni zake.
Waandamanaji walishinikiza jeshi la Marekani kuondoka
"Hii ni Agadez, sio Washington, jeshi la Marekani nendeni nyumbani," lilisomeka bango kubwa lililoinuliwa na waandamanaji. Issouf Emoud, ambaye anaongoza Vuguvugu la M62 katika mji huo, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba ujumbe wao uko wazi: "Wanajeshi wa Marekani wapakie virago vyao na kurudi nyumbani".
Soma pia: Ujumbe wa Marekani kuzungumza na utawala wa kijeshi Niger
Mwanaharakati huyo aliratibu pia maandamano ya kutaka kuondoka kwa vikosi vya Ufaransa ambavyo vilijiondoa rasmi mwaka jana. Kwa muda mrefu Niger imekuwa nchi ya mkakati kwa Marekani na Ufaransa katika azma yao ya kupambana na makundi ya kigaidi katika eneo la Afrika Magharibi.
Mwezi uliopita, Jeshi la Niger lilitangaza kuvunja makubaliano ya ulinzi na Marekani, kwa madai kuwa yalifikiwa chini ya shinikizo na kwamba kuwepo kwa wanajeshi wa Marekani nchini humo ni kinyume cha sheria.
Makubaliano kati ya Niger na Marekani ya kuondoa wanajeshi hao
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Kurt Campbell alikubali kuwaondoa wanajeshi hao katika mkutano mjini Washington na waziri mkuu wa NIger, Ali Mahaman Lamine Zeine, walieleza maafisa wa Marekani wakiliambia shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina.
Kwa upande wake kiongozi wa mashirika ya kiraia Amobi Arandishu amesema kutumwa kwa jeshi la Marekani nchini Niger "hakuna manufaa kwa usalama wao", na kusisitiza kuwa makundi yenye silaha bado yanaendelea kuzusha vurugu katika maeneo ya jangwani, na kwamba mataifa ya Urusi, Marekani, Ujerumani, Ufaransa, wote wanakuja Niger kwa maslahi yao wenyewe.
Soma pia: Ufaransa inanuia kujenga 'ubia wenye uwiano' na Afrika baada ya uhusiano kudorora
Baada ya mapinduzi yaliyomuondoa madarakani rais wa Niger aliyechaguliwa kidemokrasia Mohamed Bazoum, utawala wa kijeshi ulivitimua pia vikosi vya wakoloni wao wa zamani Ufaransa mwishoni mwa mwaka 2023.
Kuongezeka kwa ushawishi wa Urusi nchini Niger
Wakufunzi wa kijeshi wa Urusi waliwasili Niger mwezi huu wakiwa na vifaa kadhaa vya kijeshi pamoja na mfumo wa ulinzi wa anga. Hayo yalielezwa na vyombo vya habari vya serikali, hatua iliyofikiwa baada ya mazungumzo kati ya mtawala wa kijeshi Jenerali Abdourahamane Tiani na Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Kujiondoa kwa Marekani nchini humo kunaashiria ushindi mpya wa Urusi katika kuimarisha ushawishi wake barani Afrika na hususan katika ukanda huo, ambapo inaziunga pia mkono serikali za kijeshi katika nchi jirani za Mali na Burkina Faso.
Niger inakabiliwa na ghasia za makundi ya kigaidi kama Boko Haram na wapinzani wao wa Kundi la wanamgambo wa itikadi kali la Dola la Kiislamu katika kanda ya Afrika Magharibi - ISWAP kutoka eneo la kusini mashariki la Diffa karibu na Nigeria.
(Chanzo: AFP)