1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMamlaka ya Palestina

Mamia wahofiwa kuuawa kwenye shambulizi la hospitali Gaza

17 Oktoba 2023

Zaidi ya watu 500 wameripotiwa kuuawa usiku wa Jumanne kwenye shambulizi ambalo limetokea hospitalini Ahli Arab katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4Xf0C
Picha za mwanzo zikionyesha waokozi wakitoa huduma kwa wahanga wa shambulizi hilo.
Picha za mwanzo zikionyesha waokozi wakitoa huduma kwa wahanga wa shambulizi hilo.Picha: Reuters TV/REUTERS

Wizara ya afya ya Hamas imedai shambulizi la angani la Israel ndilo limesababisha maafa hayo. 

Lakini jeshi la Israel limekana kuhusika na kusema roketi ya Wanamgambo wa Kiislamu huko Gaza ndiyo imepiga hospitali.

Rais Mahmoud Abbas wa Palestina ametangaza siku tatu za maombelezo baada ya mashambulizi hayo, kwa mujibu wa mamlaka za ukanda huo.

Kulingana na Israel, intelijensia ya jeshi lake imebaini kuwa roketi iliyofyatuliwa vibaya na wanamgambo wa Gaza ndiyo ilishambulia hospitali ya Ahli Arab.

Kupitia taarifa, msemaji wa jeshi la Israel amedai kuwa tathmini ya mifumo ya operesheni ya jeshi lao inaonyesha kuwa msururu wa makombora ulirushwa na magaidi huko Gaza. Amesema makombora hayo yalipita karibu na hospitali ya Al Ahli wakati iliposhambuliwa.

"Intelijensia tulizonazo kutoka vyanzo mbalimbali, zinaonesha wanamgambo wenye misimamo mikali ya Kiislamu, ndio wanawajibika kutokana na roketi iliyofeli na kupiga hospitali.''

"Kinachoendelea sasa ni mauaji ya kimbari. Tunaitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia haraka kuzuwia mauaji haya ya maangamizi. Ukimya haukubaliki," ilisema taarifa iliyotolewa na Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO) kinachoongozwa na Abbas.

Abbas na PLO walipoteza udhibiti wa Ukanda wa Gaza kwa kundi la Hamas baada ya uchaguzi wa 2006 uliofuatiwa na mapambano makali ya kuwania madaraka.

Haya yanajiri wakati rais wa Marekani Joe Biden akitarajiwa kuizuru Israel Jumatano, siku moja baada ya ziara ya Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz mjini Tel Aviv.

Jeshi la israel limekanusha kuhusika na shambulizi la hospitali na limedai roketi iliyokosa mwelekeo baada ya kufyatuliwa na wanamgambo wa Gaza ndiyo ilipiga hospitali hiyo.
Jeshi la israel limekanusha kuhusika na shambulizi la hospitali na limedai roketi iliyokosa mwelekeo baada ya kufyatuliwa na wanamgambo wa Gaza ndiyo ilipiga hospitali hiyo.Picha: ISRAELI ARMY/REUTERS

Mashambulizi hayo ya Jumanne, 17 Oktoba 2023 yamelaaniwa vikali 

Shirika la Afya Duniani, WHO limelaani shambulizi hilo la Jumanne katika hospitali na kutaka ulinzi wa haraka kwa raia na vituo vya afya katika eneo hilo la Palestina.

"WHO linalaani vikali shambulizi katika hospitali ya Al Ahli Arab. Tunatoa wito kwa ulinzi wa haraka wa raia na huduma za afya, na amri za kuwahamisha ibadilishwe" amesema Tedros Adhanom Ghebreyesus, mkuu wa WHO, kupitia ukurasa wake wa X zamani ukijulikana kama Twitter.

Kulingana na Tedros, ripoti za awali zimesema mamia ya watu wameuawa na wengi wamejeruhiwa.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel, amesema mashambulizi dhidi ya miundombinu ya raia, haiendi sambamba na sheria ya kimataifa.

Mfalme Abdullah wa Jordan amesema shambulio dhidi ya hospitali huko Gaza ni mauaji ya "kimbari” na "uhalifu wa kivita” ambao yeyote yule hawezi kunyamazia kimya.

Wizara ya mambo ya nje ya Jordan imesema kuna haja ya watu wa Palestina kupatiwa ulinzi wa kimataifa na wakati huo huo ilitowa wito kuwepo juhudi za pamoja kuzuwia vita vinavyoendelea kwenye Ukanda wa Gaza.

Qatar imeyaita mashambulizi hayo kuwa ni "mauaji ya kikatili ya maangamizi" na uhalifu usio mfano dhidi ya raia wasiokuwa na ulinzi wowote."

Picha za kwanza kutoka nje ya hospitali iliyoshambuliwa zilionekana kuonyesha watu wengi waliokufa na kujeruhiwa
Picha za kwanza kutoka nje ya hospitali iliyoshambuliwa zilionekana kuonyesha watu wengi waliokufa na kujeruhiwaPicha: Dawood Nemer/AFP via Getty Images

Saudi Arabia pia imelaani mashambulizi hayo. Kwenye taarifa yake, wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo imesema mashambulizi hayo ni "uvunjaji wa wazi wa sheria za kimataifa."

Picha za televisheni zinaonesha mamia ya watu wakivutwa kutoka vifusi vya jengo la hospitali hiyo.

Tahadhari ya Israel kwa wakaazi wa kaskazini mwa Gaza

Jeshi la Israel liliwaambia wakaazi wa kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, takriban nusu ya idadi jumla ya watu milioni 2.4 katika ukanda huo, kuelekea kusini kwa usalama wao, kabla ya kuanza kwa mashambulizi ya ardhini.

Maelfu ya watu wamekuwa wakimiminika katika hospitali zilizofurika Gaza wakitafuta hifadhi kutokana na mashambulizi ya kijeshi ya Israel.

Guterres kwenda Misri

Israel imekuwa ikifanya mashambulizi katika Ukanda wa Gaza wakiwalenga wanamgambo wa Hamas, tangu kundi hilo lilipofanya mashambulizi makubwa ya kushtukiza dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7.

Israel, Marekani, Umoja wa Ulaya na nchi nyingine kadhaa zimeliorodhesha kundi la Hamas kuwa la kigaidi.

Zaidi ya watu 1,400 wameuawa nchini Israel kufuatia mashambulizi ya Oktoba 7 ya wanamgambo wa Hamas.

Katika Ukanda wa Gaza, zaidi ya watu 3,000 wameuawa kufuatia mashambulizi ya angani ya Israel.

Vyanzo: RTRE, AFPE, DW