1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden kuizuru Israel wakati ikijiandaa kuivamia Gaza

17 Oktoba 2023

Wapalestina wameelezea mashambulizi makali mapema Jumanne karibu na miji miwili iliyoko kusini mwa Gaza, ambako Israel iliwaamuru raia kuchukuwa hifadhi. Maelfu wamejikusanya katika kivuko cha Rafah cha kuingia Misri.

https://p.dw.com/p/4XcpD
Msaada wa kiutu wa Misri kwa ajili ya Gaza mjini Al-Arish
Watu wenye bendera za Misri wakishangilia karibu na msafara wa malori yaliobeba msaada kiutu kwa ajili ya Wapalestina, uliotolewa na mashirika yasio ya kiserikali ya Misri, Oktoba 15, 2023.Picha: REUTERS

Malori yaliyobeba mahitaji muhimu kwa ajili ya Gaza yamewasili kwenye kivuko cha Rafah nchini Misri, ambacho ndiyo njia pekee ya kuingia katika ukanda huo nje ya udhibiti wa Israel.

Shuhuda moja ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa malori takribani 60 yaliondoka kutoka mji wa karibu wa Al-Arish nchini Misri, yalikokuwa yakisubiri wakati wanadiplomasia wakijaribu kwa siku kadhaa kufungua njia.

Israel imeapa kuliangamiza vuguvugu la Hamas linalodhibiti Ukanda wa Gaza, baada ya wapiganaji wa kundi hilo kuwauwa watu 1,300, wengi wao wakiwa raia, wakati wa uvamizi wa kustukiza dhidi ya miji ya kusini mwa Israel Oktoba 7, ambao unatajwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kufanywa katika historia ya miaka 75 ya taifa la Israel.

Soma pia: Vita vya Israel-Hamas: Hali eneo la Gaza yazidi kudorora

Israel imeilenga Gaza kwa mashambulizi ya angani yaliosababisha vifo vya zaidi ya watu 2,800 na kuwafurusha takribani nusu ya wakaazi wake milioni 2.3 kutoka majumbani mwao. Pia imeiwekea Gaza mzingiro, ambao mpaka sasa umezuwia msaada wote ikiwemo chakula, mafuta na dawa.

Ukanda wa Gaza| Wapalestina wakisubiri kuvuka kivuko cha Rafah
Wapalestina wenye uraia wa nchi mbili wakisubiri nje ya kivuko cha Rafah katika matumaini ya kupata ruhusa ya kuondoka Gaza, kufuatia mzozo kati ya Israel na Hamas.Picha: Ibraheem Abu Mustafa/REUTERS

Biden kuzuru Israel kusikiliza mahitaji yake

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, akitangaza ziara ya Biden baada ya mazungumzo ya masaa kadhaa na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, alisema rais Biden atasikia kutoka kwa Israel juu ya nini inakihitaji kwa ajili ya ulinzi wa watu wake, na namna itakavyoendesha operesheni zake katika namna inayopunguza vifo vya raia na kuwezesha msaada wa kiutu kuwafikia raia wa Gaza, kwa namna ambayo haitainufaisha Hamas.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz ameelekea Israel hii leo kwa ajili ya kuonyesha mshikamano na viongozi wa taifa hilo wakati huu wakipambana na Hamas, ambayo Marekani, Umoja wa Ulaya na mataifa mengine kadhaa yanairodhesha kuwa kundi la kigaidi.

Kabla ya kuondoka kwenda Israel, Scholz amefanya mazungumzo na Mfalme wa Jordan Abdallah wa Pilii, ambapo wawili hao wamelaani mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel, huku Scholz akiihakikishia Israel kwa mara nyingine kwamba Ujerumani inasimama kikamilifu upande wake.

Soma pia: Migawanyiko ndani IMF, Benki ya Dunia kuhusu vita vya Gaza

''Nasema tena kwa mara nyingine kwa uwazi kabisa, tunalaani vikali shambulio la magaidi wa Hamas dhidi ya Israel. Israeli ina haki ya kujibu ugaidi huu. Usalama wa Israeli lazima uimarishwe tena na Ujerumani iko upande wa Israeli bila shaka yoyote. Kwa pamoja na washirika wetu sisi kama Serikali ya Shirikisho tunatumia nguvu zetu zote kuhakikisha kuwa mgogoro huu hautazidi kuongezeka,'' alisema Scholz.

Ujerumani | Kansela Olaf Scholz akimpokea Mfalme wa Jordan Abdullah II.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, akisalimiana na mgeni wake, Mfalme wa Jordan, Abdullah II, Oktoba 17, 2023, mjini Berlin, Ujerumani.Picha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Jordan, Misri kutochukuwa wakimbizi wa Palestina

Kwa upande wake Mfalme Abdullah amesema kwamba Jordan na Misri hazitachukuwa wakimbizi zaidi kutoka Palestina, akiitaja hiyo kuwa msitari mwekundu, na kuongeza kuwa ameweza kuszungumza kwa niaba ya nchi nyingine jirani na Israel kuhusu suala hilo.

Soma pia: WHO: Haiwezekani kuwahamisha wagonjwa Gaza

Israel imesema wapiganaji wa Hamas waliwachukuwa mateka watu 199 wakati wa uvamizi wao. Hamas kwa upande wake imesema wageni miongoni mwa mateka hao walikuwa wageni wao, na kwamba watawaachia pale mazingira yatakaporuhusu, huku ikibainisha wazi malengo ya kubadilisha mateka wa Israel na maelfu ya Wapalestina walioko katika jela la Israel.

Wakati Israel ikipanga uvamizi wa ardhni mjini Gaza kuwafurusha Hamas, makabiliano ya kuvuka mpaka yameongezueka na kundi la Hezbollah katika safu ya pili kwenye mpaka wa kaskazini wa Israel na Lebanon.

Chanzo: Mashirika