Miito yatolewa kuweka suluhu ya nje mzozo wa Gaza
3 Januari 2024Mpaka sasa maafisa wa Israel hawajazungumzia shambulio la Jumanne usiku, lililomuuwa Saleh Al-Arouri, afisa mwenye cheo cha juu kabisa wa Hamas kuuawa tangu kuanza kwa vita vya Gaza karibu miezi mitatu iliyopita. Msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari, alisema jeshi hilo liko katika hali ya utayari kwa ajili ya hali yoyote ile.
Hata hivyo, mkuu wa shirika la ujasusi la Mossad, David Barnea, amedokeza juu ya kuhusika kwa Israel katika mauaji ya Arouri, baada ya kunukuliwa na gazeti la Jerusalem Post akisema "Mama yeyote wa Kiarabu anapaswa kujua kwamba ikiwa mtoto wake alikuwa mshirika katika mashambulizi ya Oktoba 7, damu yake iko mikononi mwake."
Gazeti la Jerusalem Post limeyafasiri matamshi hayo ya Barnea alioyatoa katika mazishi ya mkuu wa zamani wa Mossad, Zvi Zamir, leo Jumatano, kama ishara ya wazi ya ushiriki wa Israel katika mauaji ya Al-Arouri, lakini Barnea hakumtaja kwa jina.
Soma pia: Mauaji ya kiongozi wa Hamas Beirut yazidisha hatari ya kusambaa kwa vita vya Gaza
Gazeti hilo lilisema ilikuwa inashangaza kwamba Barnea amejitokeza na tamko kwa kuzingatia ukweli kwamba Israel haijajitwika dhamana ya mauaji hayo hadharani.
Miito yaongezeka kutafuta suluhu
Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, UNIFIL, umeonya kwamba kuongezeka kwa uhasama, kutokana na mauaji ya Arouri kunaweza kuwa na madhara makubwa, na kutoa wito kwa pande zote kujizuwia, na mataifa yenye ushawishi kuingilia kati.
Mkuu wa sera ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Joseph Borrel, amesema ulimwengu unapaswa kulazimisha suluhisho kwa mzozo wa Gaza.
"Tunachojifunza sasa kutokana na janga linaloshuhudiwa Gaza ni kwamba suluhu lazima iwekwe kutoka nje," Borrell aliwamabia waandishi habari nchini Ureno.
"Amani itapatikana tu kwa njia ya kudumu ikiwa jumuiya ya kimataifa itashiriki kwa undani ili kuifanikisha na kulazimisha suluhisho," alisema akizitaja Marekani, Ulaya na mataifa ya Kiarabu.
Borrell alionya kwamba shambulio la Jumanne lililomuua Al-Arouri lilikuwa "jambo la ziada linaloweza kusababisha kuongezeka kwa mzozo."
Mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7 kusini mwa Israel yaliuwa takribani watu 1,200 na wengine wapatao 240 walichukuliwa mateka.
Mashambulizi ya angani na ardhini ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza yameua zaidi ya watu 22,100, ambapo theluthi mbili kati yao ni wanawake na watoto, kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas.
Mashambulizi ya Israel yamewahamisha takribani asilimia 85 ya wakaazi wa Gaza kutoka makazi yao, na kuwalazimu maelfu kurundikana katika makazi ya muda yaliyoja, au mahema yaliopo katika maeneo yalioanishwa na Israel kuwa salama. Robo ya wakaazi wa Gaza wanakabiliwa na hatari ya kufa kwa njaa, wakati ambapo mapigano makali yakizuwia kuwasilishwa kwa msaada.
Washirika wa Israel walaani miito ya kuwahamisha Wapalestina wa Gaza
Hayo yakijiri, mataifa washirika wa Israel, ya Marekani, Ufaransa na Ujerumani, yamekosoa vikali kauli zilizotolewa na mawaziri wawili ndani ya serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, Waziri wa Fedha Bezalel Smotrich na wa Usalama wa taifa, Itamar Ben Gvir, za kutaka Wapalestina wahamishwe kutoka Gaza na eneo hilo kukaliwa na walowezi.
Soma pia: Shambulio la Israel Lebanon lamuua naibu mkuu wa Hamas
Siku ya Jumapili, Waziri Smotrich alisema Israel inapaswa kuhimiza uhamaji kutoka Gaza na kuanzishwa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo hilo, ambako iliondoa wanajeshi wake mwaka 2005. Ben Gvir alitoa matamshi sawa na hayo kuhusu kuwahamisha Wapalestina.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya nje ya Ujerumani Sebastian Fischer, alisema Jumatano kwamba Berlin, mshirika wa karibu wa Israel, inakataa kwa nguvu zote matamshi yaliotolewa na mawaziri hao wawili, na kwamba hayana manufaa yoyote wala hayasaidii.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, pia alionya dhidi ya fikira ya kuwafukuza Wapalestina kutoka maeneo yao, akihoji katika mazungumzo ya simu la mjumbe wa Baraza la kivita Benny Gantz, kwamba matamshi yanayohusiana na kuwahamisha watu wa Gaza hayakubaliki na yanakinzana na suluhisho la mataifa mawili ambalo ndiyo pekee linalotekelezeka kwa ajili ya kurejea kwa amani na usalama kwa wote.
Utawala wa Rais Joe Biden pia ulikemea vikali miito ya mawaziri wa Netanyahu, huku msemaji wa wizara ya mambo ya nje Matthew Miller, akisema katika taarifa kwamba matamshi hayo ya Bezalel Smotrich na Itamar Ben Gvir, yalikuwa ya uchochezi na ya kutowajibika.