Rais wa Ufaransa atoa wito wa usitishwaji mapigano Gaza
28 Desemba 2023Rais Emmanuel Macron ameelezea wasiwasi wake kufuatia idadi kubwa ya vifo vya raia katika Ukanda wa Gaza ambavyo kwa sasa vimepindukia 21,000 kulingana na wizara ya afya inayodhibitiwa na Hamas.
Taarifa ya Ikulu ya Elysée imeeleza kuwa katika siku zijazo, Ufaransa itashirikiana na nchi ya Jordan ili kutekeleza shughuli za kibinaadamu huko Gaza.
Aidha Macron amesisitiza pia umuhimu wa hatua za kukomesha ukatili unaofanywa na walowezi wa Israel dhidi ya raia wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na kuzuia kuanzisha makazi mapya yanayotarajiwa eneo hilo.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Netanyahu amemshukuru Macron kutokana na jukumu la Ufaransa katika kulinda uhuru wa usafiri katika Bahari Nyekundu na "nia ya kusaidia kurejesha usalama katika mpaka kati ya Israel na Lebanon. Eneo hilo limekuwa likishuhudia vurugu katika wiki za hivi karibuni kufuatia uasi wa kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.
Soma pia:Mahmoud Abbas: Israel inaendesha vita vya maangamizi Gaza
Kaimu waziri wa mambo ya nje wa Australia Mark Dreyfus amesema hii leo kuwa raia wawili wa Australia, akiwemo Ali Bazzi anayedaiwa kuwa mpiganaji wa Hezbollah, waliuawa kufuatia shambulizi la anga la Israel siku ya Jumanne katika mji wa Bint Jbel kusini mwa Lebanon.
Madhila ya wakimbizi wa ndani Gaza na maandamano Marekani
Maelfu ya Wapalestina wamelazimika kuyakimbia makazi yao kufuatia mashambulizi ya ardhini ya Israel yanayoendelea huko Gaza. Osama Al-Zant ni mmoja wao:
" Nyumba zetu zilibomolewa, na mwanangu aliuawa. Tulikimbia huku kukiwa na mlipuko usiku kucha, tukaja hapa kutoka Khan Younis hadi Deir al-Balah, eneo lililo karibu na mashujaa wa Al-Aqsa. Hakuna malazi bora. Kila tunapokwenda eneo lolote wanatulenga huko. Tunalala nje na hatujui nini cha kufanya. Sina chakula wala maji kwa ajili ya watoto wangu. Tumekaa tu hapa bila hata kikombe cha maji."
Soma pia: Abbas: Mzozo wa Gaza ni zaidi ya kukitokomeza kizazi cha wapalestina
Nchini Marekani, kumeshuhudiwa maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina katika miji kadhaa. Polisi wa Mji wa Los Angeles wamefahamisha kuwa watu 36 wametiwa mbaroni baada ya kuzusha vurugu huku watu wengine 26 wakikamatwa mjini New York kwa kuzuia barabara kuu inayoelekea katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa John F. Kennedy.