Juhudi za Israel kuwalinda raia Gaza zatiliwa shaka
8 Desemba 2023Jeshi la Israel linaendeleza operesheni yake yenye dhamira ya kulitokomeza kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza. Mwandishi wa DW mjini Jerusalem Tania Krämer amezungumza kwa njia ya simu na wakaazi wa Gaza ambao walimueleza kuwa hawana mahali pa kwenda wakati Israel ikipanua operesheni zake za ardhini kuelekea eneo la kusini mwa Gaza.
Krämer amesema raia wa Gaza wamemweleza kwamba iwapo hakutakuwepo wito wa usitishwaji kamili wa mapigano, hawewezi kubakia salama huko Gaza. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya inayodhibitiwa na Hamas, zaidi ya Wapalestina 17,000 wameuawa tangu Israel ilipoanzisha hujuma zake mnamo Oktoba 7 kujibu shambulizi kubwa lililofanywa na kundi la Hamas ndani ya ardhi yake. Shambulizi hilo liliwauwa watu 1,200 nchini Israel. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa karibu watu milioni 1.9, ikiwa ni asilimia 80 ya wakaazi wa Gaza, wameyakimbia makaazi yao kutokana na makabiliano yanayoendelea.
Hayo yakijiri, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken, ametilia shaka juhudi zinazofanywa na Israel kuwalinda raia huko Gaza. Hiyo ni kauli ya kwanza ya ukosoaji mkubwa wa operesheni za Israel ambayo imetolewa na afisa wa ngazi ya juu wa serikali ya Marekani tangu kuanza kwa vita hivyo Oktoba 7.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Washington, Blinken amesisitiza kuwa Israel inapaswa kuzingatia ulinzi wa raia lakini akabainisha wazi kwamba bado kuna tofauti kubwa kati ya nia ya kuwalinda raia na matokeo halisi ambayo yanashuhudiwa.
Akishiriki mkutano huo na wanahabari akiwa na mwenzake Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Cameron, ambaye yupo ziarani nchini Marekani amesema:
" Tunasimama pamoja nanyi katika kuiunga mkono Israel na haki yake ya kujilinda na kuhakikisha kwamba wanakabiliana na kundi la kigaidi la Hamas ambalo lilifanya mauji ya kutisha Oktoba 7, wakati huo huo tunatilia mkazo umuhimu wa kutii sheria ya kimataifa ya kibinaadamu na kujaribu kupunguza vifo vya raia."
Wapalestina wauawa Ukingo wa Magharibi
Wizara ya Afya ya Palestina imesema hii leo kuwa takriban Wapalestina sita wameuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel kwenye kambi ya wakimbizi ya Al-Fara karibu na mji wa Tubas unaopatikana huko Ukingo wa Magharibi, eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel.
Shirika la Habari la Palestina, WAFA, limeripoti kuwa Wapalestina hao wameuawa katika makabiliano na wanajeshi wa Israel ambao walivamia kambi hiyo huku kukiripotiwa mashambulizi makali na milipuko. Jeshi la Israel limesema linachunguza taarifa hiyo.
Soma pia: Wapiganaji wa Hamas waelezwa kuishambulia Isreal
Mamlaka ya Palestina imeeleza kwamba takriban Wapalestina 263 wameuawa kwenye eneo la Ukingo wa Magharibi tangu Oktoba 7, ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya vifo ikilinganisha na mwaka jana. Wanajeshi wa Israel na walowezi wa kiyahudi ndiyo wanaolaumiwa kwa vifo hivyo.
Leo hii, Umoja wa Falme za Kiarabu umeliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuipigia kura rasimu ya azimio ambayo inapendekeza kusitishwa mara moja kwa mapigano kati ya Israel na Hamas kwa sababu za kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.
Ili kupitishwa kwa azimio hilo, kutahitajika angalau kura tisa za uungwaji mkono na kusiwepo kura hata moja ya turufu kutoka kwa wanachama watano wa kudumu wa Baraza hilo ambao ni Marekani, Urusi, China, Ufaransa au Uingereza. Hata hivyo, Marekani imesema kwa wakati huu, haiungi mkono hatua yoyote ya ziada ya baraza hilo.