1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Iran zahimizwa kurejelea makubaliano ya nyuklia

15 Desemba 2021

Umoja wa Mataifa umeihimiza Marekani kuondoa vikwazo ilivyoiwekea Iran kama ilivyoainishwa katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, huku ukiitaka Iran kurejea katika utekelezaji kamili wa makubaliano hayo.

https://p.dw.com/p/44JIk
Österreich Gebäude des Hauptsitzes der Internationalen Atomenergie-Organisation (IAEA)
Picha: Michael Gruber/Getty Images

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kisiasa na upatikanaji wa amani, Rosemary DiCarlo, ameitaka  Marekani kuondoa vikwazo hivyo pamoja na kurefusha muda wa msamaha kuhusu biashara ya mafuta na Iran.

DiCarlo ameyasema haya katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakati majadiliano yakiendelea mjini Vienna kujaribu kuyafufua makubaliano ya pamoja ya utekelezaji wa mpango wa nyuklia unaofahamika kama JCPOA.

soma zaidi: Israel yataka Iran isilegezewe masharti kuhusu nyuklia

Mjumbe huyo ameongeza kwamba, kurefushwa kwa msamaha kunahitajika ili kuondoa madini ya urani yaliyorutibishwa na kutoa nafasi ya kuwepo kiwango kinachohitajika kwa matumizi ya kiraia pekee.

Katika taarifa ya pamoja Ujerumani, Uingereza, Ufaransa,Urusi na China mataifa yalio na nguvu yaliosehemu ya makubaliano hayo, wamesema milango ya kidiplomasia iko wazi kwa Iran kuheshimu makubaliano ya sasa.

Iran inabidi ichague ama kuanguka kwa makubaliano ya JCPOA au makubaliano ya sasa kwa manufaa ya watu wa Iran na taifa hilo kwa ujumla.

Marekani: Yajitayarisha kuingia kikamilifu katika makubaliano ya nyuklia

USA I US Botschafterin Linda Thomas-Greenfield I UN
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Linda Thomas-GreenfieldPicha: Luiz Rampelotto/EuropaNewswire/picture alliance

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Majid Takht Ravanchi amesema kurejea tena katika utekelezaji wa makubaliano hayo, taifa lake halijaweka matakwa yoyote kwa hilo kufanyika na hatua zote ilizochukua baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano inaweza kugeuzwa.

Mwenzake wa Marekani, Linda Thomas-Greenfield, amesema Marekan inajitayarisha kuingia kikamilifu katika makubaliano hayo akitumai Iran pia ina nia ya kufanya vivyo hivyo.

Majadiliano ambayo sio ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani yanayosimamiwa na mataifa ya ulaya yalianza tena mwezi Novemba mjini Vienna kwa nia ya kuyaokoa makubaliano ya mwaka 2015 yaliyonuiwa kuizuwiya Iran kufikia na kupata silaha za nyuklia.

soma zaidi: Mazungumzo ya kufufua mkataba wa nyuklia wa Iran kuanza tena

Makubaliano hayo yamekuwa yakiyumba kuanzia mwaka 2018 wakati rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alipoiondoa nchi hiyo katika makubaliano hayo, yaliyoiondolea Iran vikwazo kwa nia ya kuachana na mpango wake wa nyuklia.

Hata hivyo baadae Marekani ilivirejesha vikwazo vya uchumi Iran hatua iliyofanya taifa hilo lijibu kwa kukiuka viwango vya urutubishaji wa madini ya urani vilivyokuwa vimewekwa chini ya makubaliano ya mwaka 2015. Rais Joe Biden ameonyesha nia ya kuirejesha Marekani katika makubaliano hayo.

Chanzo: afpe