Marekani na Kenya zatia saini makubaliano ya ulinzi
26 Septemba 2023Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na Waziri wa Ulinzi wa Kenya Aden Duale wametia saini makubaliano hayo katika mkutano uliofanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.
Makubaliano hayo ni mwongozo wa maswala ya ulinzi wa nchi ya Kenya kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Hayo yanatokea wakati ambapo eneo la Afrika Mashariki limeongeza kasi ya vita dhidi ya kundi la Al Shabaab lenye mahusiano na kundi la kigaidi la al-Qaeda.
Waziri Austin ameishukuru Kenya kwa kujitolea kukiongoza kikosi cha mchanganyiko wa maafisa kutoka mataifa mbalimbali cha kulinda usalama nchini Haiti.
Amesisitiza ahadi ya serikali ya Marekani ya kuipa Kenya ufadhili wa dola milioni 100 ilizoahidi kwenye mkutano uliofanyika kandoni mwa mkutano uliomalizika mjini New York wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Soma pia:Haiti na Kenya zaanzisha uhusiano wa kidiplomasia
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin ameihimiza jumuiya ya kimataifa kuiga mfano wa Kenya kwa kutoa maafisa zaidi, vifaa, wasaidizi, mafunzo na ufadhili wa fedha.
Kenya imeahidi kuwapeleka maafisa 1,000 wa usalama nchini Haiti kupambana vurugu zinazoendeshwa na magenge ya wahalifu.
Ujumbe huo unasubiri kibali rasmi kutoka kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Hadi sasa nchi hiyo tayari imepata idhini ya awali kutoka kwa Umoja wa Mataifa na Marekani.
Waziri wa ulinzi wa Kenya Aden Duale amesema nchi yake iko tayari kuwapeleka maafisa wake nchini Haiti.
Duale ameitaja historia ndefu ya ulinzi wa amani duniani ya Kenya kuanzia nchini Kosovo, katika nchi Jirani ya Somalia na katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Hata hivyo wanaharakati wa haki za binadamu, wameelezea wasiwasi wao juu ya kupelekwa askari wa Kenya nchini Haiti.
Wanaharakati hao wamekumbusha juu ya ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa operesheni za usalama za ndani ya nchi.
Soma pia:Magenge yenye silaha nchini Haiti yataka serikali ipinduliwe
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya usalama nao wameeleza wasiwasi wao.
Wamesema kutakuwa na kikwazo cha lugha kati ya maafisa kutoka Kenya taifa linalozungumza lugha za Kiingereza na Kiswahili na watu wa Haiti ambako lugha zinazotumika ni Kifaransa na Creole.
Chanzo:AP