1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSyria

Marekani na Urusi zafanya mashambulizi Syria

13 Novemba 2023

Urusi na Marekani zimefanya mashambulizi tofauti nchini Syria na kuwalenga wapiganaji wenye silaha. Wapiganaji 34 wameuawa na Urusi kwenye Jimbo la Idlib, huku wapiganaji 8 wakiuawa na Marekani mashariki mwa Syria.

https://p.dw.com/p/4YjgG
Türkei | Incirlik Air Base US Kampfjet F-16
Ndege ya kivita ya Marekani (F-16) ikiondoka katika uwanja wa Incirlik nchini Uturuki ili kupambana na kundi la kigaidi IS (12.08.2015)Picha: Krystal Ardrey/U.S. Air Force via AP/picture alliance

Jeshi la Marekani limefanya shambulio la tatu la anga katika kipindi cha wiki kadhaa nchini Syria na kulenga kituo cha mafunzo cha wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran karibu na mji wa Albu Kamal na eneo lao la makazi ya waasi hao karibu na mji wa Mayadeen.

Shirika la Kutetea Haki za Kibinadamu la Syria limesema wapiganaji wanane wanaoiunga mkono Iran, wakiwemo angalau watu wawili raia wa Syria na Irak ndio waliouawa katika  mashambulizi ya Marekani mashariki mwa Syria.

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin akiwa mjini Seoul nchini Korea Kusini amesema leo kuwa kuna uwezekano wa kuendelea na mashambulizi zaidi dhidi ya makundi yenye mafungamano na Iran ikiwa mashambulizi dhidi ya majeshi ya Marekani huko Irak na Syria hayatositishwa.

Soma pia:Marekani yafanya mashambulizi Syria 

Mashambulizi hayo yanajiri baada ya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran kuwashambulia angalau mara 40 wanajeshi wa muungano wa Marekani nchini Iraq na Syria, katika wakati mvutano wa kikanda ukiongezeka kufuatia vita vya Israel na kundi la Hamas. Takriban wanajeshi 45 wa Marekani wamejeruhiwa.

USA | Anhörung des Senats Lloyd Austin
Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd AustinPicha: Getty Images

Marekani ina jumla ya wanajeshi 900 nchini Syria, na wengine 2,500 katika nchi jirani ya Iraq, ili kusaidia vikosi vya ndani kujaribu kuzuia kuibuka tena na kuimarika kwa kundi la kigaidi linalojiita  Dola la Kiislamu IS,  ambalo mnamo mwaka 2014 lilinyakua maeneo makubwa katika nchi zote mbili lakini baadaye likatokomezwa.

Wasiwasi umekuwa ukiongezeka kwamba mzozo wa Israel na Hamas unaweza kutanuka katika eneo zima la Mashariki ya Kati na hivyo kambi za wanajeshi wa Marekani kulengwa na mashambulizi ya silaha nzito au ndege zisizo na rubani.

Tangu kuibuka kwa mzozo kati ya Israel na Hamas  Oktoba 7, Marekani imeimarisha ulinzi wa anga na kutuma meli na ndege za kivita katika eneo hilo kujaribu kuzuia makundi yanayoungwa mkono na Iran. Maelfu ya wanajeshi walioongezwa pia katika eneo hilo.

Mashambulizi ya Urusi nchini Syria

Syrien Bashar Al-Assad
Rais wa Syria Bashar al-Assad (Picha ya mwaka 2015)Picha: Sana/Handout/dpa/picture alliance

Urusi pia imefanya mashambulizi nchini Syria na kuwaua wapiganaji 34 na kuwajeruhi wengine wapatao 60 katika jimbo la Idlib. Mamlaka ya jeshi la Urusi imesema mashambulizi hayo yamevilenga vikundi haramu vyenye silaha ambavyo vimekuwa mara kadhaa vikishambulia vikosi vya serikali ya Syria. Katika muda wa masaa 24 yaliyopita,  vikosi vya syria vimeshambuliwa mara saba.

Jeshi la Syria limekanusha kuwalenga na kusema mashambulizi hayo katika mikoa ya Idlib na Aleppo huendeshwa na makundi yenye misimamo mikali ya kiislam. Lakini viongozi wa upinzani wanasema Moscow na Damascus zinatumia fursa hii wakati macho ya ulimwengu yakielekezwa katika mzozo wa Gaza, ili kuongeza shinikizo katika maeneo ambayo zaidi ya watu milioni tatu wamekataa kuishi chini ya utawala wa kimabavu wa Rais wa Syria Bashar al-Assad.

(Vyanzo: AFPE,RTRE)