1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Urusi zaligawa baraza la Usalama

13 Machi 2012

Malumbano kati ya Marekani na Urusi kuhusu mgogoro wa Syria yamekwamisha juhudi za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuafikiana juu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuumaliza mgogoro huo.

https://p.dw.com/p/14JjS
Mgogoro wa Syria umeligawa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Mgogoro wa Syria umeligawa Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: REUTERS

Marekani, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ziko msitari wa mbele kuzitaka Urusi na China kuunga mkono azimio la baraza la usalama la umoja wa mataifa linalolaani ukandamizaji nchini Syria, ambao kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa umewaua watu zaidi ya 7,500 mnamo mwaka mmoja uliopita.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary Clinton amesema Marekani haiamini kuwa kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine kuna maana kuwa baraza la usalama linapaswa kubakia kimya, wakati serikali ya Syria ikiuwa watu wake, na kuyumbisha usalama wa eneo zima. Pia amesema kuwa matendo ya upinzani hayawezi kuwekwa kwenye uzani mmoja na ukandamizaji wa serikali.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary Clinton
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary ClintonPicha: dapd

''Tunapinga kutaka kulinganisha mauaji ya makusudi, yanayofanywa na jeshi la serikali, na hatua za raia waliozingirwa, wanaolazimika kujilinda.'' Alisema Clinton.

Mazungumzo ndilo suala la msingi

Lakini, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Sergey Lavrov amejibu shinikizo hilo lililotolewa kwenye kikao maalum kujadili vugu vugu la mageuzi katika ulimwengu wa kiarabu, kwa kusema kuwa muda wa mwisho unaowekwa na nchi za magharibi hautafanikiwa. Lavrov alisema suala lenye kipaumbele ni mazungumzo ya kusimamisha ghasia.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Sergey Lavrov
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi, Sergey LavrovPicha: AP

''Kuna muafaka unaozidi kupata nguvu, juu ya umuhimu wa kuleta pande zinazohasimiana kwenye meza ya mazungumzo, ambayo msingi wake si kusema ndio au hapana, si ulipizaji kisasi wala kutoa adhabu, bali kuzingatia maslahi ya watu wa Syria. Ili hilo lifikiwe lazima ghasia zisitishwe mara moja, kama suala la msingi.'' Alisema Lavrov.

Mwakilishi wa China Li Baodong amesema hakutakuwa na uingiliaji wa kijeshi ndani ya Syria, na kukanusha shutuma kuwa nchi yake ilitumia kura yake ya turufu ikiongozwa na maslahi yake binafsi.

Wito wa kuongea kwa sauti moja

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amesema anaungana na mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu Syria, Kofi Annan, kumhimiza rais wa Syria kuchukua hatua za haraka mnamo siku chache zijazo, kulingana na mapendekezo yaliwekwa na Kofi Annan.

Mwakilishi wa UN na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu Syria, Kofi Annan
Mwakilishi wa UN na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu Syria, Kofi AnnanPicha: AP

''Naomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuongea kwa sauti moja, kuunga mkono wito wa Kofi Annan wa kukomeshwa kwa ghasia, na kuinusuru Syria kutumbukia katika janga kubwa zaidi.'' Alisema Ban Ki Moon.

Wanadiplomasia wamebaini kuwa Rais Bashar al Assad ana muda hadi leo Jumanne kutoa jibu lake kwa mapendekezo ya Kofi Annan. Akizungumza kabla ya kuondoka nchini Syria, Kofi Annan alisema ametoa mapendekezo thabiti kwa Rais Assad, yanayotaka kusitishwa kwa umwagaji damu, na kufungua njia ya msaada wa kibinadamu katika miji yenye harakati za upinzani.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Allain Juppe, amesema Rais Assad alikubali kutoa jibu lake katika muda wa masaa 48. Wanadiplomasia wanabashiri kwamba itachukua wiki kadhaa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuweza kupitisha azimio lake la kwanza juu ya mgogoro wa Syria ambao umedumu kwa zaidi ya mwaka mzima.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE

Mhariri: Yusuf Saumu