Marekani na Uturuki kuijadili Mashariki ya Kati
7 Desemba 2009Mazungumzo hayo yanakuja mnamo wakati ambapo Marekani inairai Uturuki kuwa na mchango mkubwa zaidi katika suala la Afghanistan kwasababu ya nafasi yake ya kuwa msimamizi wa operesheni za kulinda amani za NATO.
Wakati huohuo msuluhishi wa Ujerumani katika mzozo wa Mashariki ya Kati Ernst Uhrlau yuko Israel ili kuiwasilishia serikali mapendekezo ya Hamas ya kubadilishana wafungwa.
Mchango wa Uturuki
Rais wa Marekani Barack Obama na Waziri Mkuu huyo wa Uturuki watajadiliana juu ya hali katika mashariki ya kati.
Aidha Rais Obama anataka kuungwa mkono na Uturuki katika suala la Afghanistan wakati ambapo mivutano bado inaendelea kati ya mataifa wanachama wa NATO na Mashariki ya Kati.Uturuki ina umuhimu mkubwa katika suala la Afghanistan kwani ndilo taifa pekee la kiislamu lililochangia wanajeshi wake katika jumuiya ya kujihami ya NATO.Hata hivyo kabla ya kuelekea Marekani,Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisisitiza kuwa nchi yake imeshachangia wanajeshi wa kutosha katika kikosi cha NATO.Uturuki ilichukua uenyekiti wa zamu wa operesheni za kulinda amani za NATO mwezi uliopita na ikaongeza maradufu idadi ya wanajeshi wake hadi 1750. Wanajeshi hao wanahusika na majukumu ya kushika doria mjini Kabul.
Uturuki iliyo mwanachama wa NATO imekataa kuvipeleka vikosi vyake kushiriki katika mapambano dhidi ya wapiganaji wa kiislamu ukizingatia kuwa imekuwa na uhusiano wa kihistoria na Afghanistan.Rais Obama na Waziri Mkuu Erdogan watayajadili masuala ya Iraq,Pakistan na vita dhidi ya ugaidi,mtikisiko wa kiuchumi ulimwenguni na nishati.Baada ya kikao cha Washington Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ataelekea Mexico kwa ziara ya siku tatu atakakokutana na Rais Felipe Calderone.
Saa 48 ni muhimu
Kwa upande mwengine duru za Hamas zinaeleza kuwa kipindi cha saa 48 zijazo ni muhimu katika suala la kubadilishana wafungwa na Israel.Matamshi hayo yametolewa pindi baada ya msuluhishi wa Ujerumani Ernst Uhrlau kuwasili mjini Tel Aviv ili kuiwasilishia serikali ya Israel mapendekezo yake ya kubadilishana wafungwa.Wakizungumza na Kituo cha Televisheni cha Al Jazeera,maafisa wa Hamas walisisitiza kuwa wameipa Israel kipindi cha saa 48 kuliridhia dai lao la mamia ya wafungwa wa Palestina kuachiwa ndipo wamuachie huru mfungwa wa Israel Gilad Shalit.
Baada ya kukutana na maafisa wa Israel mjumbe huyo wa Ujerumani anatarajiwa kurejea katika Ukanda wa Gaza kwa minajili ya kukutana na wawakilishi wa Hamas wanaolidhibiti eneo hilo.Shalit alikamatwa na wanajeshi wa Hamas mwaka 2006 katika eneo linalopakana na Gaza.Mazungumzo ya kuachiwa ambayo si ya moja kwa moja yaliyoshika kasi yamekuwa yakisimamiwa na Ujerumani na Misri.Waziri wa Mambo ya nje wa Misri Ahmed Abul Gheit aliilaumu Israel kwa kuichelewesha hatua hiyo ya kubadilishana wafungwa kwani inaendeleea kukataa kuwaachia baadhi ya wafungwa wa Palestina.
EU kuingilia kati
Wakati huohuo Mfalme Abdullah wa pili wa Jordan ameutolea wito Umoja wa Ulaya kuingilia kati ili kuishawishi Israel kusitisha ujenzi wa makazi ya Jerusalem.Kauli hizo zimetolewa wakati ambapo mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanajiandaa kukutana mjini Brussels.Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitangaza kuwa ujenzi wa makazi mapya ya Wayahudi katika eneo la Ukingo wa Magharibi utasitishwa ila uamuzi huo haulihusishi eneo la Jerusalem Mashariki.
Mwandishi:Thelma Mwadzaya –RTRE/AFPE
Mhariri:Aboubakary Liongo