Marekani: Uchaguzi wa Uganda ulikuwa na kasoro nyingi
21 Februari 2016Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Mark Toner amesema katika ujumbe wake usiku wa kuamkia leo, kwamba ingawa uchaguzi wa Alhamisi nchini Uganda kwa kiasi kikubwa ulikuwa wa amani, mchakato wa upigaji kura na taratibu zinazoambatana na zoezi hilo viliendeshwa katika mtindo ambao haukidhi viwango vya kimataifa na matarajio ya kidemokrasia.
Aidha, msemaji huyo alitoa wito wa kuachiwa haraka kiongozi wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye kutoka kizuizi cha nyumbani.
Miongoni mwa mambo yasio ya kawaida aliyoyataja Mark Toner kucheleweshwa kwa vifaa vya upigaji kura katika vituo, ripoti kuhusu makaratasi ya kura ambayo yaliwasilishwa yakiwa tayari na alama za uchaguzi, ununuzi wa kura, uzuiaji wa mitandao ya kijamii na matumizi ya nguvu za ziada kwa upande wa jeshi la polisi.
Wapinzani wadai Museveni ni mtawala wa kijeshi
Akizungumza baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza Museveni kama mshindi, Besigye ambaye kwa mujibu wa matokeo rasmi alipata asilimia 35.4 ya kura zote, amesema hawayakubali matokeo hayo.
''Tumeyakataa matokeo ya uchaguzi huu, hatutashirikiana na utawala wa kijeshi, utawala huo hauwezi kuendelea bila ushirikiano wetu, kwa hiyo, kuweni imara, kwa kudra za mwenyezi mungu tutashinda''. Amesema kwa ghadhabu Besigye.
Lakini madai hayo ya upinzani yamepuuzwa na chama tawala, NRM ambacho kimesema ushindi wa mgombea wao, Yoweri Museveni, umedhihirisha kwamba wapinzani wake wameshindwa kuonyesha kwamba wanaweza kuleta tofauti yoyote mbali na kutoa ahadi tupu.
Mmoja wa maafisa wa NRM Mike Sebalu, amesema vyama vyote vilikuwa na wawakilishi katika ofisi za kuhesabu kura, na madai ya mizengwe ni kisingizio tu.
Sebalu amesema, ''Haya madai ya kuwepo udanganyifu ni njia mojawapo ya walioshindwa kuhalalisha kushindwa kwao, wakikaidi kutambua kwamba kunaweza kuwa kumetokana na udhaifu wao wa ndani, na mipangilio ya vyama vyao.''
Sio Kizza Besigye pekee aliyeukosoa uchaguzi huu..mgombea mwingine wa upinzani, waziri mkuu wa zamani Amama Mbabazi ambaye pia aliwekwa katika kizuizi cha nyumbani lakini baadaye akaachiwa huru, amesema matokeo ya uchaguzi huo hayaendi sambamba na matakwa ya wananchi wa Uganda.
Hata waangalizi waelezea wasiwasi
Hali kadhalika, waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya wamesema uchaguzi wa wiki hii nchini Uganda umeendeshwa katika mazingira ya unyanyasaji kwa wagombea na kwa wapiga kura. Ujumbe wa Jumuiya ya Madola vile vile umesema uchaguzi huo haukuheshimu misingi muhimu ya kidemokrasia.
Mpiga kura mmoja mjini Kampala, Brenda-binti mwenye umri wa miaka 23 ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba anasikitika kumekuwepo wizi wa kura, na kuongeza ''Sijamuona Rais mwingine maishani mwangu, na inavyoelekea itaendelea hivi hadi Museveni atakapofariki''.
Museveni ameiongoza Uganda kwa miaka 30 na ameleta utengamano baada ya miaka mingi ya ghasia nchini humo, lakini wapiga kura wa upinzani wanamshutumu kwa kuimarisha utawala wa kiimla, na kuonyesha azma ya kuwa Rais wa maisha.
Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre/afpe
Mhariri:Caro Robi