1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Marekani, Ufaransa zaapa kuiwajibisha Urusi kwa vita Ukraine

2 Desemba 2022

Marais wa Marekani na Ufaransa wamesema wataiwajibisha Urusi kwa matendo yake nchini Ukraine, huku Umoja wa Ulaya ukitangaza ukomo kwa bei ya mafuta ya Urusi ili kuibania Moscow mapato ya kufadhili vita vyake Ukraine.

https://p.dw.com/p/4KP4X
Joe Biden und Emmanuel Macron in Washington
Picha: Jonathan Ernst/REUTERS

Rais Joe Biden pia alisema atakuwa tayari kuzungumza moja kwa moja na Rais wa Urusi Vladmir Putin kuhusu kumaliza vita, lakini akaongeza kuwa hakuna dalili bado ya hili kutokea.

Mnamo Machi, mwezi mmoja baada ya kuanza kwa uvamizi wa Urusi, Biden alimuita Putin katili, kuhusiana na hatua zake na kusema kiongozi huyo wa Kremlin hawezi kusalia madarakani.

Soma pia: Urusi yakasirishwa na Ufaransa kuunga mkono korti ya uhalifu

Na sasa, baada ya miezi tisa ya mapigano na huku msimu wa baridi ukizidi kutia fora, mataifa ya magharibi yanajaribu kuimarisha msaada wa Ukraine wakati ikikabiliana na madhara ya mashambulizi ya makombora na droni yaliyowaacha mamilioni bila joto la majumbani, umeme na maji.

 Joe Biden and Jill Biden with French President Emmanuel Macron and  Brigitte Macron
Marais Joe Biden na Emmanuel Macron pamoja na wake zao katika roshani ya chuma cha Bluu cha Ikulu ya White House, wakati wa hafla ya kuwasili Houte House Alhamisi, Desemba 1, 2022.Picha: Patrick Semansky/dpa/picture alliance

Biden alisema baada ya mkutano wake na Macron mjini Washington, kwamba mataifa hayo pamoja na washirika watasimama kidete dhidi ya ukatili wa Urusi.

"Na tutaendeleza uungwaji mkono mkubwa kwa watu wa Ukraini wanapotetea makazi yao, na familia zao, na bustani zao, hospitali zao, uhuru wao, uhuru wa mamlaka yao dhidi ya uvamizi wa Urusi," alisema Biden.

Urusi imezishtumu Marekani na NATO kwa kutoa mchango wa moja kwa moja na wa hatari katika vita hivyo na kusema Washington imeigeuza Kyiv kuwa kitisho kwa uwepo wa Moscow, jambo ambalo haingeweza kulipuuza.

Putin yuko tayari kwa mazungumzo: Kremlim

Alipoulizwa kuhusu kauli ya Rais wa Marekani Joe Biden kwamba atafanya mazungumzo na Putin tu ikiwa Urusi itaondoka Ukraine, msemaji wa Kremlin Dymtri Peskov amesema leo kuwa Putin mara zote amekuwa tayari kwa mazungumzo, lakini matakwa ya rais Biden yatafanya mazungumzo kutowezekana.

Soma pia: Ukraine: Tunahitaji mifumo ya ulinzi ya anga ya Marekani

"Rais wa Shirikisho la Urusi amekuwa na bado yuko tayari kwa mazungumzo ili kuhakikisha masilahi yetu. Bwana (Joe) Biden alisema nini? Alisema mazungumzo yanawezekana tu ikiwa Putin ataondoka Ukraine kwanza. Bila masharti, operesheni maalum ya kijeshi inaendelea."

Mapigano yameendelea kupamba moto mashariki mwa Ukraine, ambapo mji wa Bakhmut umekuwa shabaha ya mashambulizi ya makombora ya Moscow, huku vikosi vya Urusi katika mikoa ya kusini ya Kherson na Zaporizhzhia vikishambuliwa, kulingana na kamandi kuu ya jeshi la Ukraine.

Kreml Sprecher  Dmitry Peskow
Msemaji wa Rais Putin, Dmitry Peskov amesema Putin yuko tayari kwa mazungumzo lakini siyo kwa sharti la kuondoa majeshi Ukraine.Picha: ITAR-TASS/IMAGO

Katika jaribio la kupunguza fedha zinazomitika kufadhili vita vya Moscow, Umoja wa Ulaya umefikia makubaliano ya awali jana Alhamisi kuweka ukomo wa dola 60 kwa pipa la mafuta kutoka Urusi, kwa mujibu wa wanadiplomasia.

Hatua hiyo hata hivyo itapaswa kuidhinishwa na serikali zote za mataifa ya Umoja wa Ulaya.

Scholz amhimiza Putin kutafuta suluhsisho la kidiplomasia

Katika hatua nyingine Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amefanya mazungumzo na Rais Putin leo Ijumaa kutafuta suluhisho la dilomasia kwa vita nchini Ukraine, ikiwemo kuondoa wanajeshi, Berlin imesema kufuatia simu kati ya viongozi hao wawili.

"Kansela amemhimiza rais wa Urusi kufikia haraka iwezekanavyo suluhisho la kisiplomasia ikiwemo kuondoa wanajeshi wa Urusi," kwa mujibu wa msemaji wa kiongozi huyo wa Ujerumani Steffen Hebestreit.

Soma pia: Umeme warejea kwenye maeneo karibu yote ya Kiev

Wakati wa mazungumzo yao ya simu yaliodumu kwa saa moja, Scholz "alilaani hasa mashambulizi ya anga ya Urusi dhidi ya miundombinu ya kiraia nchini Ukraine na kusisitiza azma ya Ujerumani kuisaidia Ukraine katika kuhakikisha uwezo wake wa kiulinzi dhidi ya uvamizi wa Urusi."

Miji 40 ya Ukraine yashambuliwa kwa makombora ya Urusi

Viongozi hao pia wamejadilia suala la usalama wa chakula duniani, ambao unakabiliwa na shinikizo kutokana na vita hivyo.Wamekubaliana "kuendeleza mawasiliano", amesema Hebestreit.

Scholz na Putin wamekuwa wakifanya mazungumzo ya simu ya mara kwa mara wakati wote wa vita.

Simu ya mwisho kati yao ilifanyika Septemba na ilidumu kwa dakika 90, ambapo Scholz pia wakati huo alimsihi Putin "kufikia suluhisho la kidiplomasia haraka iwezekanavyo, lenye msingi wake katika kusitisha mapigano.