1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaYemen

Marekani yaharibu makombora 14 ya waasi wa Kihouthi

18 Januari 2024

Jeshi la Marekani limefanya mashambulizi na kuharibu makombora 14 ya Wahouthi yaliyopangwa kurushwa kutoka Yemen, katika duru ya nne ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya kundi hilo la waasi chini ya muda wa wiki moja.

https://p.dw.com/p/4bPEG
Waasi wa Houthi wakionyesha makombora yao ya masafa marefu mjini Sanaa, Yemen
Waasi wa Houthi wakionyesha makombora yao ya masafa marefu mjini Sanaa, YemenPicha: Mohammed Mohammed/Xinhua News Agency via picture alliance

Katika taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa X, Kamandi Kuu ya jeshi la Marekani eneo la Mashariki ya Kati imeeleza kuwa makombora hayo ya Wahouthi yalinuiwa kutumika kushambulia meli za wafanyibiashara na meli za kijeshi za Marekani katika bahari ya Sham.

Kamandi ya jeshi la Marekani eneo la Mashariki ya Kati CENTCOM imesema makombora 14 ya Wahouthi yalinuiwa kurushwa wakati wowote na katika hali ya tahadhari, jeshi hilo lilifanya kile ilichoeleza kuwa ni haki na wajibu wao wa kujilinda.

Soma pia: Rais wa Iran alaani mashambulizi ya Marekani dhidi ya Wahouthi 

Marekani imeongeza kuwa, mashambulizi hayo pamoja na hatua nyingine za kiusalama zilizochukuliwa na jeshi lake, kwa kiasi kikubwa itaadhoofisha uwezo wa Wahouthi na kupunguza makali yao ya kuendelea kuzishambulia meli za biashara katika bahari ya Sham, ghuba ya Aden na mlango wa bahari wa Bab-el-Mandeb.

Mapema jana, Kamandi Kuu ya jeshi la Marekani ilisema kuwa shambulio la droni iliyorushwa kutoka maeneo yanayodhibitiwa na waasi hao wa Houtthi ililenga meli inayomilikiwa na Marekani katika ghuba ya Aden.

Houthi waishambulia meli ya Marekani ya Genco Picard

Meli ya Marekani ya USS Maron
Meli ya Marekani ya USS MaronPicha: U.S. Navy/ZUMA/picture alliance

Kupitia mtandao wa X, jeshi hilo limeandika kuwa, kulikuwepo na uharibifu lakini hakuna majeruhi yoyote yaliyoripotiwa.

Hujuma zinazofanywa na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran dhidi ya meli katika bahari ya Sham tangu mwezi Novemba kwa kiasi fulani zimepunguza kasi ya biashara kati ya bara Asia na Ulaya na pia kuzitia wasiwasi nchi zenye uchumi mkubwa duniani. Aidha, mashambulizi hayo ya Marekani yanapania kupunguza makali ya Wahouthi katika bahari ya Sham.

Waasi wa Kihouthi ambao wanadhibiti sehemu kubwa ya Yemen, mara sio moja, wameweka wazi kuwa wanafanya mashambulizi hayo kama sehemu ya kuonyesha mshikamano na Wapalestina katika ukanda wa Gaza na wametishia kutanua mashambulizi yao.

Soma pia: Marekani na Uingereza zashambulia waasi wa Yemen 

Yahya Sarea ni msemaji wa Wahouthi, "Katika kuiunga mkono Palestina na kuonyesha mshikamano na ndugu zetu katika ukanda wa Gaza, na kujibu uchokozi wa Marekani na Uingereza dhidi ya nchi yetu, jeshi letu la wanamaji limefanya mashambulio yaliyolenga meli ya Marekani ya Genco Picard katika ghuba ya Aden. Mashambulizi hayo yalilenga shabaha, tunamshkuru Mungu."

Haya yanatokea katikati ya uamuzi wa Marekani wa kuwarudisha waasi wa Houthi katika orodha ya makundi ya kigaidi.

Maafisa wa Marekani wamesema hatua hiyo inalenga kukata mizizi ya ufadhili na silaha wanazopokea Wahouthi na ambazo baadaye wanazitumia kuzishambulia au kuziteka nyara meli.

Hata hivyo, licha ya makombora yao 14 kuharibiwa na mashambulizi ya Marekani, waasi Wahouthi wamesema hawajakata tamaa na kwamba mapambano yataendelea.