Marekani yatoa tahadhari tena juu ya Urusi kuivamia Ukraine
11 Februari 2022Kauli hiyo ameitoa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken siku ya Ijumaa akisema Urusi inakusanya wanajeshi zaidi kwenye mpaka wa Ukraine, na kuonya kuwa huenda uvamizi huo ukafanyika wakati Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi ikiwa inaendelea.
Akizungumza katika mkutano wa habari mjini Melbourne kufuatia mkutano wa kundi lisilo rasmi la Quad, linalozijumlisha Marekani, Australia, India na Japan, Blinken amesema uvamizi unaweza kuanza wakati wowote huku akipuuza maoni kwamba Moscow ingelisubiri hadi Michezo ya Beijing imalizike ili kuepuka kumkwaza mshirika wake China.
Blinken amesisitiza kwamba Marekani ingependelea mno kutatua tofauti hizo na Urusi kwa njia ya kidiplomasia na kwamba wamefanya kila juhudi kuishirikisha Urusi. Lakini wakati huo huo, amesema wamekuwa wawazi katika kujenga vizuizi na kuimarisha ulinzi huku wakiitahadharisha wazi Urusi kwamba ikiwa itachagua njia ya uvamizi mwengine, basi itakabiliwa na matokeo makubwa.
Blinken amesema nchi kadhaa zimeanza kutafakari kuhusu hatua dhidi ya Urusi endapo itaivamia Ukraine.
"Nchi kadhaa zimeliweka wazi hili pia. Nchi zote za G7 zimejiunga pamoja, nchi zenye nguvu na za kidemokrasia duniani, zimeweka wazi kwamba matokeo makubwa yatafuata kutokana na uvamizi mwengine. Vivyo hivyo kwa Umoja wa Ulaya, na hata NATO."
Kauli hizo zinakuja wakati Rais Joe Biden katika mahojiano na kituo cha habari cha NBC News, amewataka raia wa Marekani waliopo nchini Ukraine kuondoka mara moja nchini humo, ikiwa ishara nyingine kwa umma kwamba vita huenda vipo mlangoni.
Picha za satelaiti zilizochapishwa na kampuni ya Marekani zinaonyesha vikosi vya Urusi vikipelekwa katika maeneo kadhaa karibu na Ukraine, na kueleza kuwa majeshi hayo yanaendelea kujizatiti eneo hilo huku kukiwa na msururu wa mikutano ya kidiplomasia yenye lengo la kutuliza mgogoro huo.
Urusi inafanya pia mazoezi ya kijeshi katika nchi zilizokuwa zamani katika muungano wa Kisovieti kama Belarus pamoja na mazoezi ya majini katika Bahari Nyeusi. Kuongezeka kwa harakati za kijeshi karibu na Ukraine kumezua hofu ya uvamizi. Urusi imekuwa ikikanusha mara zote mipango yoyote ya kumshambulia jirani yake.
Wakati huohuo Finland ambayo inapakana na Urusi itatia saini makubaliano ya dola bilioni 9.4 siku ya Ijumaa ili kununua ndege za kivita kutoka Marekani wakati ambapo Moscow inatishia hatua za kijeshi ikiwa jumuiya ya NATO haitawaondoa wanajeshi wake mashariki mwa Ulaya.