1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marufuku ya kutembea usiku yatangazwa Lamu

6 Januari 2022

Serikali ya Kenya imetangaza marufuku ya kutembea usiku kwa siku 30 katika baadhi ya maeneo ya jimbo la Lamu, kufuatia mashambulizi ya kigaidi yaliosababisha vifo vya watu na makaazi kuteketezwa.

https://p.dw.com/p/45BYU
Türkei Antalya 2021 | Uhuru Kenyatta, Präsident
Picha: Metin Aktas/Anadolu Agency/picture alliance

Agizo hilo linajiri siku moja baada ya vyombo vya usalama kuanzisha msako wa kuwakamata wavamizi hao. Kwa mujibu wa taarifa hiyo maeneo yatakayoathiriwa na kafiu hiyo ni pamoja na: Mukunumbi, Majembeni, Ndamwe, Mkunumbi, Witu, Pandanguo, Binde Warinde, Hamasi, Mpeketoni, Bomani, Pongwe, Mpeketoni, Bahari, Mapenya na Lamu Central.

Hali ya wasiwasi inazidi kushuhudiwa katika eneo hilo ambalo limekuwa likishambuliwa mara kwa mara. Mama Hellen alimpoteza mumewe, siku ya Jumatatu kwenye uvamizi wa saa kumi alfajiri.

Mbali na hayo, waziri Mating'I amesema kuwa Baraza la Usalama wa Taifa limeagiza kupelekwa mara moja kwa vyombo vya usalama kukusanya silaha haramu na kudumisha utangamano.

Wakazi wa maeneo yaliyoathiriwa wametakiwa kushirikiana na vyombo hivyo vya usalama kwa kutoa habari ambazo zitasaidia kukamatwa kwa wavamizi hao. Taarifa hiyo ya serikali imesema kuwa visa vya uhalifu vimesababisha mauaji ya watu saba wasio na hatia katika kijiji cha Widho kata ya Majembeni katika jimbo la Lamu.

Wanajeshi wa Kenya wamekuwa wakikabiliana na kundi la al shaabab tangu mwaka 2014, linaloaminika kuyatekeleza mashambulizi hayo.

Je ya kutembea nje usiku ndio suluhisho?

Afrika, Nairobi Verschärfter Corona-Lockdown
Mwendesha pikipiki akipita katika barabara za Nairobi, Kenya wakati wa masharti ya kutotoka nje usikuPicha: Boniface Muthoni/zumapress.com/picture alliance

Mchambuzi wa masuala ya usalama George Musamali, wavamizi hao hawana mafungamano yoyote na kundi hilo la kigaidi wala Kafiu sio mwarubaini wa usalama katika jimbo hili la Lamu.

Mashambulizi ya Jumatatu na Jumanne yanafanana na mashambulizi yaliyotokelezwa mwaka 2014 na 2015 katika eneo la Mpeketoni na Hindi, jimbo hilo la Lamu. Katika mashambulizi hayo, wavamizi waliwafunga waathiriwa mikono kwa nyuma kabla ya kuwakata koo. 

Kwa mujibu wa polisi watu watano kati ya saba waliouawa walikuwa wamefungwa mikono kabla ya kukatwa vichwa.

Aidha wavamizi hao waliteketeza nyumba za waathiriwa. Hali ya taharuki inayoshuhudiwa sasa imewalazimisha baadhi ya wakazi kuanza kuhama.

Uvamizi huu sio tu pigo kwa usalama lakini pia utalii ambao unategemewa na wakazi wa eneo hilo.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Dw, Nairobi