Mashirika 65 yataka kuachiwa kwa waandishi wa Burundi
23 Oktoba 2020Waandishi hao ni Agnes Ndirubusa, Christine Kamikazi, Egide Harerimana na Terence Mpozenzi. Walikamatwa pamoja na dereva wao kwenye mkoa wa Bubanza, Oktoba 22 mwaka jana.
Waandishi hao walishikiliwa na polisi wakati walipokuwa wakiendesha uchunguzi wao kuhusu mashambulizi ya kundi la waasi la RED-Tabara lililo kwenye mpaka wa Burundi na Kongo.
Soma pia: Amnesty, waandishi wasio mipaka walaani kufungwa wanahabari Burundi
Dereva wao Adoplhe Masabarakiza aliachiwa huru baadaye,lakini waandishi hao walihukumiwa mwezi Januari kwa kifungo cha miaka miwili na nusu jela kwa kuhatarisha usalama wa nchi. Kifungo ambacho kilithibitishwa na mahakama ya rufaa mwezi Juni.
"Tunalaani hukumu hiyo isiyo ya haki na tumeomba kuachiwa huru haraka kwa wenzetu. Ikiwa mahakama haiwezi kuwaachia huru, kwa sababu hawakufanya kosa lolote, basi tunamuomba rais wa nchi kufanya kila awezalo ili kuwapa msamaha wa rais ili wenzetu hao wawe huru," alisema mkuu wa shirika la habari la Iwacu, Leandre Sikayavuga.
Kifungo bila ushahidi?
Mashirika hayo 65 ya kutetea haki za binadamu na uhuru wa habari, yakiwemo Amnesty International na Human Rigths Watch yamesema kwenye kesi ya waandishi hao mwendesha mashtaka hakutoa ushuhuda hata mmoja unaoonyesha kwamba waandishi habari hao walikuwa na ushirikiano na kundi la uasi.
Shirika la haki za waandishi habari la CPJ, lile la Waandishi Habari Bila Mipaka RSF na mengine mengi yamesema kwenye taarifa yao kwamba kushikiliwa kwa waandishi hao kunaendelea kwa tuhuma zisizo kuwa na msingi wowote, licha ya mageuzi wa uongozi nchini Burundi.
Soma pia: HRW yataka Burundi imuachie Nibitanga
Shirika la habari la Iwacu,ni moja ya vyombo vichache huru vya habari vilivyosalia nchini Burundi baada ya machafuko ya kisiasa ya mwaka 2015.
Mashirika ya haki za binadamu yamesema kuhukumiwa huko kwa waandishi habari ni ujumbe wa mahakama ya Burundi wa kuwatisha waandishi habari wengine ili wasifanye kazi yao kama kawaida.
Shirika la Waandishi wa Habari Bila Mipaka, linaiweka Burundi kwenye nafasi ya chini ya 159 kwenye orodha ya uhuru wa habari duniani.
Chanzo: AFP, DW