Matamshi ya Jenerali Otafire kuutikisa utawala wa Museveni?
19 Februari 2024Kulingana na baadhi ya wanasiasa na wadadisi, jenerali huyo anafichua kuhusu mkakati wa kumrithisha mwanawe Rais Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, lakini pia wanampongeza kuwa kudhihirisha kuwa hata yeye hafurahii hali ya mambo.
Akiwa kwenye kumbukumbu za mauaji ya aliyekuwa askofu mkuu wa Kanisa la Kianglikana, Janan Luwum, mwishoni mwa wiki, Waziri huyo wa masuala ya ndani alikaririwa na vyombo vya habari akisema "tahadharini kuhusu wale wanaowahadaa kwamba sisi ndiyo tutakuwa suluhu kwa shida zenu, wanajitakia makuu na singependa kuitumbikiza nchi hii katika hali mbaya ya utawala wa kiimla."
Soma pia:Vuguvugu la MK la Uganda lajigeuza asasi ya kiraia
Matamshi ya jenerali huyo yamefasiliwa kuwa yanalenga kuwaonya Waganda kuhusu hila na mkakati wa utawala kumtegenezea njia mwanawe Rais Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kumrithi babake.
Kulingana na mdadisi wa mambo ya kisiasa John Kibego, onyo na tahadhari za jeneralihuyo zinatakiwa kutiliwa maanani kwani ni ishara kuwa kuna hila za utawala wa sasa kupokeza kwa kiongozi ambaye hatakuwa mwenye tija kwa taifa hilo la Afrika mashariki.
"Jenerali Otafire ametufichulia hali ilivyo na sasa tunatakiwa kuchukua tahadhari kuhusiana na viongozi wanaotaka kutwaa madaraka." Alisema mchambuzi huyo wa masuala ya kisiasa mjini Kampala.
Upande wa pili wa shilingi wakosoa matamshi ya Jenerali
baadhi ya wafuatiliaji wa siasa za Uganda wamekosoa hadharani matamshi ya kuongozi huyo, kuwa nae ni sehemu ya utawala huo uliokaa mamalakani kwa zaidi ya miaka 38.
Wameongeza kuwa naye anawajibika katika mapungufu ya utawala ya kuwaweka raia hasa vijana katika mashaka kuhusu mustakabali wao. Ni kwa ajili hii ndipo inakuwa rahisi kwa wao kushawishika na kupotoshwa na wanasiasa wanaojitakia makuu.
Soma pia:Museveni atimiza miaka 38 madarakani akililia ufisadi
"Umekuwa sehemu ya utawala ambao umewatumbukiza watu katika hali ya mashaka na umasikini na kwa hiyo hata wewe unawajibikia makosa ya utawala." Asha Nantongo mwanasiasa chikupikizi aliiambia DW.
Jenerali Otafire ni waziri wa ngazi ya juu na amekuwa katika nyadhifa mbalimbali za utawala huu kwa muda mrefu akiwa arifu mkubwa wa rais Museveni. Kinachosubiriwa ni kuona jinsi rais Museveni atakavyoitikia matamshi yake ambayo kwa wengi yanaonyesha msimamo wa jenerali huyo dhidi ya hali ya sasa ya kisiasa.