1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matatizo ya uchafu wa maji katika jiji la Kampala.

19 Agosti 2008

Upatikanaji wa maji kwa ajili ya wakaazi milioni mbili katika jiji la Kampala nchini Uganda uko hatarini kutokana mipango mibaya ya miji na mabadiliko ya majira ya mvua.

https://p.dw.com/p/F0aD

Upatikanaji wa maji kwa ajili ya wakaazi milioni mbili wa mji mkuu wa Uganda , Kampala unatishiwa na mchanganyiko wa mambo kama mipango mibaya ya miji na mabadiliko ya majira ya mvua katika eneo hilo. Maji kwa ajili ya wakaazi wa mji wa Kampala yanapatikana kwa njia ya mabomba yanayomilikiwa na shirika la taifa la maji safi na maji taka, NWSC pamoja na vijito vya asili katika maeneo kadha ya mji huo. Vyanzo vyote hivyo vinakabiliwa na uchafuzi wa maji.

Kwa mujibu wa profesa Oweyegha Afunaduula , mwanaharakati wa ulinzi wa mazingira na profesa katika idara ya hifadhi ya wanyama katika chuo kikuu cha Makerere, mji wa Kampala umejikuta katika hali ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa bila kujitambua. Profesa huyo amesema kuwa jiji hilo linapata mvua ambazo hazitabiriki na hali hii imeuweka wazi mji huo ambao umepangwa vibaya kuweza kukabiliana na athari hizo.

Milima inayozunguka mji huo imejengwa nyumba ambazo zinakaa watu matajiri na maji yanayotoka katika nyumba za wakaazi hao yanayotiririka kutoka milimani hayana maeneo ya asili ya kuyanyonya na mvua kubwa zikinyesha hatimaye hutiririkia katika mabonde.

Profesa huyo amesema kuwa hii inaongeza sababu za mafuriko katika maeneo ya mabondeni , ambako wakaazi masikini ambao hawamudu kuishi katika maeneo ya milimani wamejenga nyumba zao.

Afunaduula anasema kuwa kinyesi kinaingia katika mfumo wa maji kwasababu mifereji mingi ya maji taka inaingia bila maji yake kusafishwa katika ziwa Viktoria kupitia katika mfereji wa Nakivubo, mfereji mkubwa wa maji taka ambao unapitia katikati ya jiji la Kampala. Eneo chepechepe la Nakivubo, ambalo limekuwa likitumika kama chujio la asili la maji taka , linazidi kupungua kutokana na kutumiwa na wakaazi wa mji huo kama sehemu ya kuishi.

Hali ya jiji la Kampala ni ya kutatanisha kutokana na ukweli kwamba ni asilimia 8 tu ya wakaazi wa mji huo wanapata huduma ya mabomba ya maji taka , inayotolewa na shirika la taifa la maji taka na maji safi, NWSC.

Wengi wa wakaazi wa mji huo wanatumia vyoo vya shimo, ama katika nyakati fulani hutumia mifuko ya plastiki ambayo hutupwa katika maeneo ya kutupia taka ama vijito vya maji.

Ripoti nyingine iliyotolewa na kitengo cha Kawempe cha halmashauri ya mji wa Kampala , imefichua kuwa kiasi kikubwa cha maji ya mji huo pia si safi. David Ssemwanga, mkaguzi wa afya wa kitengo hicho, anasema kuwa sampuli zilizochukuliwa kutoka maji ya bomba katika wilaya ya Kawempe, kata za Bwaise 2 , Mulago 2 na Kyebando yameonekana kuwa na bakteria wa kinyesi. Hii inaonyesha uchafuzi wa maji yanayotumiwa kutokana na kinyesi cha wanyama ama binadamu kinachoingia katika mfumo mzima wa maji.

Viwango vikubwa vya bakteria hao husababisha kipindupindu, kuharisha na ugonjwa wa matumbo, , anasema Robert Odongo, mkaguzi wa mazingira katika wizara ya afya nchini Uganda. Matukio ya kipindupindu yamekwisharipotiwa mjini Kampala , wakati baadhi ya wakaazi wanalalamikia matatizo ya tumbo. Esther Arego, mkaazi wa kitongoji kingine cha Kampala , cha Kinawataka, anaamini kuwa maji kutoka kijito cha Mukwano ambayo anayatumia si salama , lakini hana njia nyingine.

►◄