1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mateka 13 wa Israel na watoto waachiwa kutoka Ukanda wa Gaza

24 Novemba 2023

Mateka wanawake wa Israeli na watoto wameachiwa kutoka Ukanda wa Gaza leo Ijumaa (24.11.2023) kufuatia makubaliano ya kusimamisha mapigano kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas.

https://p.dw.com/p/4ZPvt
Israel Tel Aviv | watu wakishangilia kuachiwa kwa mateka
Mapokeo ya watu wa Israel baada ya taarifa kuachiwa kwa matekaPicha: Ariel Schalit/AP/picture alliance

Mateka hao 13 wa Israel wameachiwa pamoja na mateka wengine 12 raia wa Thailand.

Kwa mujibu wa mkuu wa kitengo cha habari za serikali nchini Misri, mateka hao wanatarajiwa wakati wowote kutoka sasa kupita kwenye kivuko cha Rafah kati ya Gaza na Misri.

Wakati huo huo Israel inatarajiwa kuwaachia wafungwa 39 wa Kipalestina.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameelezea matumaini kuwa mapatano ya kusitisha mapigano yaliyoanza kufanya kazi kati ya Israel na Hamas yataruhusu kupelekwa msaada katika eneo la kaskazini mwa Gaza kwa mara ya kwanza baada ya wiki kadhaa.

Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu maswala ya kibinadamu OCHA, Jens Laerke, amesema malori kadhaa yenye bidhaa yanaendelea kuvuka mpaka kuelekea Gaza.

Soma:Mpango wa usitishwaji mapigano kati ya Israel na Hamas waaanza kutekelezwa

Licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas kuanza kutekelezwa majira ya saa moja asubuhi siku ya Ijumaa,  jeshi la Israel limesisitiza juu ya kurejesha operesheni yake dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza mara baada ya kumalizika siku nne za kusimamisha mapigano.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amekariri haki ya kujilinda taifa la Israel.

Misaada ya kiutu kiutu yaingia Gaza

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Misri malori 200 ya misaada yameingia Gaza kupitia kivuko cha mpaka wa Rafah kilichopo kusini mwa ukanda huo wa pwani.

Misri imesema malori hayo 200 ya misaada yataingia Gaza kila siku wakati huu wa usitishaji wa vita, ikiwa ni pamoja na lita 130,000 za dizeli na malori manne ya gesi

Malori yalio na misaada ya kiutu yakiingia Gaza
Malori yalio na misaada ya kiutu yakiingia GazaPicha: Said Khatib/AFP

Jeshi la Israel limesema malori manne yaliyobeba mafuta na mengine manne yaliyobeba gesi yamekabidhiwa kwa mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa katika mpaka wa Rafah katika Ukanda wa Gaza.

Usafirishaji huo umeidhinishwa na serikali ya Israeli kama sehemu ya kusitisha mapigano.

Soma:Qatar imesimama kama mpatanishi mkuu katika mazungumzo ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza

Wakati huo huo, shirika linalotoa huduma za ambulensi la Hilali Nyekundu, limesema magari 10 ya kubeba wagonjwa yamepelekwa kaskazini mwa Gaza kuwahamisha wagonjwa.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yalifikiwa baada ya wiki nzima ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yaliyosimamiwa na Qatar, Marekani na Misri.

Israel ilitangaza vita dhidi ya Hamas wiki saba zilizopita baada ya wanamgambo wa Hamas kuwashamulia na kuwaua takriban watu 1,200 nchini Israel mnamo Oct. 7.

  Israeli ilijibu kwa mashambulizi makubwa ya anga na ardhini ambayo yamesababisha uharibifu kwenye maeneo makubwa katika eneo la Gaza. Wapalestina wasiopungua 13,300 wameuawa hadi kufikia sasa.

Mzozo wa Mashariki ya Kati wakaribia mwezi mmoja