Matumaini yafifia mkutano wa WTO Bali
4 Desemba 2013Waziri wa biashara wa India katika mkutano huo amesema makubaliano yoyote yanayojumuisha kuondolewa kwa ruzuku hizo hayakubaliki kwa sababu yanahatarisha sekta ambayo ni muhimu kwa sekta inayowawezesha kujikimu mamilioni ya wakulima masikini.
Hatua hiyo ya India imevuruga matarajio ya mkurugenzi mkuu wa Shirika la Biashara Ulimwenguni, WTO, Roberto Azevedo, ambaye alitumai mkutano huo unaoendelea katika mji wa Bali nchini Indonesia, ungeafiki juu ya mpango wa kibiashara ambao ungezisogeza mbele juhudi za miaka 12 kuondoa vikwazo vya kibiashara duniani.
Fursa ya mwisho
Washirki katika mkutano huo, mmoja baada ya mwingine, walikuwa wameonya kwamba huenda hii ilikuwa nafasi ya mwisho kunusuru mpango wa WTO kuweka mazingira bora ya kibiashara ulimwenguni yenye kuzingatia kwa hali iliyo sawa maslahi ya nchi tajiri na zile zinazoinukia kimaendeleo.
Kufikiwa kwa makubaliano yoyote kulitegemea kwa kiasi kikubwa msimamo wa India kuhusu usalama wa chakula. Nchi hiyo, mwezi Agosti ilipitisha sheria ya kihistoria, ambayo inairuhusu serikali kununua chakula kutoka kwa wakulima kwa bei iliyowekewa ruzuku, na kisha kukiuza chakula hicho kwa watumiaji kwa bei ya chini zaidi. India inahofia kuwa makubaliano katika mkutano huo ambayo yanataka ruzuku kwa mazao ya kilimo isizidi kiwango cha asilimia 10, yanaweza kutatiza mpango wake wa kuwapatia chakula mamilioni ya raia wake masikini.
Serikali ya nchi hiyo inayokabiliwa na uchaguzi mwaka kesho, haiwezi kuiondoa ruzuku hiyo, kwa hofu ya vyama vya upinzani na vyama vya wakulima vyenye ushawishi mkubwa.
Hali ya kukata tamaa mkutanoni
Mwakilishi wa Marekani katika mkutano wa Bali Michael Froman amesema kuambulia patupu kwa mkutano huo, kutaudhoofisha uwezo wa WTO kama baraza la kimataifa la majadiliano. Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na biashara Karel de Gucht amewaambia waandishi wa habari mjini Bali, kuwa licha ya kuwa mtu mwenye kuweka matumaini mbele, anakiri kuwa sasa amekata tamaa.
Shirika la Biashara Ulimwenguni, WTO lilianzisha kile kinachojulikana kama mazungumzo ya Doha mwaka 2001, ikiazimia kuufanyia marekebisho mfumo wa biashara ulimwenguni, kwa kuondoa vizuizi. Lakini malumbano yenye msingi wa kimaslahi baina ya nchi tajiri na masikini, na msisitizo wa WTO kuwa makubaliano yoyote lazima yaafikiwe kwa pamoja, vimeyafanya mazungumzo hayo yashindwe kupiga hatua muhimu.
Mkuu wa WTO, Roberto Azevedo amekataa kutoa kauli yoyote juu ya msimamo wa India, akisema bado kazi inaendelea.
Wataalamu wanakadiria kuwa mazungumzo ya Doha yangeweza kutoa mamilioni ya nafasi za ajira, na kurahisisha shughuli za kiuchumi zenye thamani ya mabilioni ya dola.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/APE
Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed