1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri Tanzania kujadili sakata la tozo ya miamala

Hawa Bihoga 19 Julai 2021

Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa atakutana na mawaziri kujadili kwa kina suala la tozo za miamala ya simu ambayo imezusha gumzo nchini humo kwamba inaongeza ukali wa maisha.

https://p.dw.com/p/3whS8
ElfenbeinküsteMobile Money Orange Money
Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Mjadala mpana kuhusu tozo za miamala ya simu uliodumu kwa zaidi ya siku tano sasa, huku wengi wakionekana kutokubaliana na tozo hiyo ya mshikamano ndio sababu kubwa ya Waziri Mkuu kukutana na mawaziri wenye dhamana ili kujadili kwa kina baadhi ya kanuni na hatimae kuja na ufumbuzi wa changamoto hiyo ambayo tayari imeteteresha utaratibu wa utumaji fedha kwa simu.

Waziri wa fedha na mipango Mwigulu Nchemba, amesema tayari bunge limekwishapitisha sheria na jambo linalofuata ni utekelezwaji wake, isipokuwa kuna baadhi ya maeneo ya kikanuni yanasalia upande wa waziri na hicho ndicho kitakachojadiliwa kwa kina ili kuleta muafaka kwa pande zote baina ya serikali na walipa kodi.

Aidha waziri huyo ambae ni mara ya kwanza kutoka hadharani tangu tozo hizi zimeanza kukatwa kwa kila muamala juma lililopita, ameongeza kuwa, kwa sasa wataendelea kutolea ufafanuzi kadri utavyohitajika, huku akitahadharisha dhidi ya  utopotoshaji juu ya tozo hiyo.

Kassim Majaliwa waziri mkuu wa Tanzania
Kassim Majaliwa waziri mkuu wa TanzaniaPicha: Büro des Premierministers von Tansania

Kwa mujibu wa waziri wa mawasiliano ya teknolojia ya habari Faustine Ndugulile hadi mwezi Decemba 2020 kadi za simu milioni 51 zimesajiliwa na asilimia 48.6 kati ya hizo zinafanya miamala mbalimbali, hatua inayotafsiriwa na wachumi kwamba hayo ni mapinduzi chanya katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

Tozo ya miamala ya simu bado kizungumkuti

Hata hivyo wadadisi wanaonya juu ya  sheria ya mapato iliopitishwa katika bunge lililopita yenye matokeo ya kuzaliwa kwa tozo ya miamala ya simu kwa hoja kuwa, kodi hiyo licha ya kuelekezwa katika kuboresha huduma za kijamii lakini inakiuka kanuni za kimataifa kwani mlipa kodi analipa mara mbili katika muamala mmoja, hivyo kutaka iondolewe.

Hadi sasa wafanyabiashara wengi wa mtandaoni wameamua kubadili mfumo wa malipo na kuingia katika benki, kutokana na wateja wao kulalama juu ya makato makubwa katika miamala.

Kikao cha waziri mkuu Kassim Majaliwa na mawaziri wengine ni matokeo ya Rais Samia Suluhu kuwaagiza kushughulikia malalamiko yanayoendelea kuvuma kutokana na tozo hiyo iliotokana na sheria ya kodi iliopitishwa na bunge katika bunge la bajeti lililopita.