1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa EAC wapo Zanzibar kutatua migogoro ya kikanda

8 Julai 2024

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa mataifa yanayounda Jumuiya ya Afrika Mashariki wapo visiwani Zanzibar kujaribu kutatua migogoro ya kisiasa na hali ya uhasama inayoshuhudia miongoni mwa baadhi ya nchi wanachama.

https://p.dw.com/p/4i12L
Signing ceremony of the treaty of accession by the Federal Republic of Somalia into EAC
Picha: Presidential Press Unit Uganda

Mawaziri wa mambo ya nje na wasaidizi wao kutoka nchi nane zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanakutana Zanzibar wakati huu wa changamoto nyingi za kisiasa, kijamii na kiuchumi duniani na kwenye kanda hiyo.  Mkutano huo unafanyika wakati Kenya moja ya nchi wanachama imeshuhudia wimbi kubwa la maandamano ya vijana dhidi ya serikali. 

Naibu Waziri Mkuu na waziri wa Afrika Mashariki wa Uganda, Rebecca Kadaga, na Waziri Kiongozi wa serikali ya Kenya Musalia Mudavadi ni miongoni mwa washiriki wa mkutano huo ambao ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na marais wa nchi hizo kwa mawaziri hao wakutane kwa faragha kutafuta namna bora ya kuimarisha amani, usalama na kuharakisha muungano wa kisiasa baada ya mafanikio kuanza kuonekana katika forodha na Uhuru wa kibiashara.

Rais William Ruto wa Kenya aahidi mabadiliko baada ya maandamano

Wakizungumza kando na mkutano huo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Veronica Mueni Nduva amesema mkutano huo ni wa kuulizana na kuelezana ukweli.

"Mawasiliano yetu yatakuwa ni ya uwazi na tunayaweka mambo yote mezani ikiwemo vipi tunavyoweza kurekebisha mambo ambayo hayaendi vizuri na vipi tunaweza kuuboresha umoja ambao ni thabiti, mambo ambayo yameletwa katika mkutano wa mawaziri na mkutano wa marais wanaoziwakilisha jumuiya, lakini ubunifu wa mkutano huu ni tofauti ambao utakuwa wa uwazi na kuangaliana macho kwa macho ana kwa ana na kuulizana masuali magumu," alisema Bi Nduva.

Wakitoa salaamu zao wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa siku tatu, mawaziri kutoka Burundi, Uganda, DRC, Somalia, na Kenya wamesema kuwa amani, usalama, na muungano wa kisiasa ni mambo yanayohitaji kuwekewa mikakati ili kufikia mafanikio.

Suala la vita vya Mashariki ya Kongo pia lipo katika ajaenda ya mazungumzo

DR Kongo | Waasi wa M23
Baadhi ya wanachama wa kundi la waasi wa M23 Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Mkutano huo wa faragha utawapa nafasi mawaziri hao wa kuzungumza kwa uwazi zaidi kama anavyoeleza Waziri wa mambo ya nchi na ushirikiano wa Afrika Mashariki Tanzania, January Makamba.

"Kwa sababu masuala haya ni nyeti yanahitaji utulivu yanahitaji busara na yanahitaji hekima katika kutajadili na ndio maana tukaja kujificha huku Zanzibar ili tupate kuyajadili," alisema Makamba.

Mbali ya masuala ya jumla, mkutano huo umeshuhudia pia mataifa yaliyotumbukia kwenye uhasama yakikaa mezani kujaribu kutafuta suluhu. Waziri wa mambo ya kigeni wa Rwanda Olivier Nduhungirehe alikutana na naibu waziri wa mambo ya nje wa Kongo Gracia Yamba kuzungumzia mvutano kati ya Kongo na Rwanda. Katika ujumbe wake kupitia mtandao wa kijamii wa X Ndihungirehe amesema mazungumzo na mwenzake wa Kongo yalifanyika katika hali ya nia njema na yalikuwa ya uwazi.

UN: Vikosi vya Rwanda vyasaidiana na M23 kupigana Kongo

Hata hivyo hakuna maelezo zaidi yaliyotolewa juu ya kile kilichoafikiwa. Kongo na Rwanda zimo kwenye mvutano unaotanuka kutokana serikali ya Kinshasa kuutuhumu utawala mjini Kigali kuchochea machafuko mashariki mwa Kongo, Tuhuma ambazo Rwanda mara kadhaa imezikanusha. Mkutano huo ambao umewashirikisha mawaziri wote wan chi hizo unatarajiwa kumalizika leo jioni na kutoka na maazimio mahsusi ambayo yanatazamiwa kupelekwa kwa maraisi wote wa Afrika Mashariki.

Mashambulizi ya kushtukiza katika mji wa Sake, Kongo

Mwandishi: Salma Said DW Zanzibar