Maziko ya waliouwawa na kundi la ADF yafanyika Beni
21 Novemba 2019Mauwaji yanayoendeshwa na ADF wakati operesheni dhidi ya kundi hilo la uasi ikiendelea, yanadhaniwa na wengi kuwa huenda yakavunja uhusiano ulioko baina ya jeshi na wakaazi.
Wanachama wa mavuguvugu mbalimbali ya vijana wameandamana, kuomboleza jamaa waliopata msiba pamoja na kupinga mauwaji ya kila uchao katika wilaya ya Beni.
Wakizungumza na DW katika njia panda kuu ya Beni Nyamwisi, vijana hao ambao waliwapatia wanajeshi wa tume ya Umoja wa mataifa Monusco ilani ya masaa 48, ili wawe wameondoka Beni huku wakisema hawaoni sababu ya wanajeshi hao kuwepo na ikiwa bado wanauwawa.
Wadadisi wengi wa masuala ya usalama katika eneo hili, wanadhani kwamba, mauwaji yanayoendelea pamoja na mgomo na maandamano ya leo, huenda yakavunja ndoa iliyoko kwa sasa, baina ya majeshi ya serikali yaliyoko kwenye uwanja wa mapambano katika misitu.
Mauaji hayo yazidi kuwatia huzuni wakaazi wa Beni
Maoni hayo hata hivyo yanatupiliwa mbali na baraza la wazee wa busara wa mji wa Beni, wanaodhani kwamba, maandamano pamoja na mgomo, ni aina fulani ya wakaazi kuomboleza na familia zilizopata msiba, na katu hayawalengi wanajeshi walioko kwenye operesheni dhidi ya waasi kutoka Uganda ADF.
Ifahamike kuwa, waasi wa ADF waliwauwa watu sabaa katika mji wa Beni na wengine kumi na wanne katika kijiji cha Mavette wilayani Beni, kilomita thelathini na sita Kaskazini Magharibi mwa mji wa Beni.
Wahanga wa mauwaji ya juzi mjini Beni, wanazikwa, wakati wakaazi wa Beni wakiwa na uchungu moyoni.
Tangu yalipoanza mauwaji ya wakaazi kwa kukatwa kwa mapanga na ADF, raia wasiopungua elfu tatu wameshapoteza maisha yao,kulingana na takwimu zinazotangazwa na mashirika ya kiraia.
Chanzi: John Kanyunyu DW Beni