Mazungumzo ya kusaka maridhiano Kenya kuanza Jumatano
7 Agosti 2023Wakenya sasa watasubiri zaidi kuona ufanisi wa mazungumzo ya maridhiano yanayolenga kuzika tofauti kati ya serikali na upinzani, baada ya kikao cha leo (Julai 7) kuvunjika.
Hali hiyo inaibua wasiwasi kwenye taifa ambalo watu 30 wameshauawa kwenye maandamano yaliyoongozwa na upinzani kwa majuma mawili.
Kutokana na mvutano wa mahali mazungumzo hayo yatakapofanyikia, imebidi yaahirishwe hadi siku ya Jumatano kulingana na duru kutoka pande zote mbili.
Soma zaidi: Kenya yahitimisha siku ya tatu ya maandamano
Kambi za kisiasa Kenya kuchuana kuwania uspika
Vyama vyote bado havijakubaliana kuhusu masuala yanayozua utata.
Huku upinzani ukitaka suala la gharama ya maisha kujadiliwa, upande wa serikali ya Kenya Kwanza umekataa ukisema kuwa hiyo ni ajenda ya serikali.
Aidha upinzani unataka matokeo ya uchaguzi yakaguliwe tena, suala ambalo Kenya Kwanza imesema kuwa mahakama ya juu ilishafanya uamuzi.
Ajenda nyengine muhimu
Baadhi ya hoja kwenye ajenda ya mazungumzo hayo ni pamoja na uundaji upya wa Tume ya Kusimamia Uchaguzi, utekelezaji wa kanuni ya jinsia mbili kwa thuluthi mbili, kuimarisha mfuko wa maendeleo ya majimbo, kuundwa na kuimarishwa kwa ofisi ya kiongozi wa upinzani, na kuwekwa kwa ofisi ya Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri.
Kiongozi wa serikali bungeni Kimani Ichung'wah atawaongoza wajumbe wa kikosi cha Kenya Kwanza, wakati kikosi cha upinzani cha Azimio kitaongozwa na kiongozi wa chama cha Wiper na aliyekuwa Makamu wa Rais, Kalonzo Musyoka.
Soma zaidi: Serikali ya Kenya kwanza kukabiliana na vitisho
Kalonzo ajiunga tena na kikosi cha Azimio One Kenya
Lakini hata kabla ya mazungumzo yenyewe kuanza, tayari hapo siku ya Jumapili (Julai 6) kiongozi mkuu wa upinzani, Raila Odinga, alisema kuwa iwapo mazungumzo hayo "hayatafanyika na kuzaa matunda yoyote katika kipindi cha siku 30," basi atawangoza wafuasi wake kwenye maandamano mapya.
Kwa upande wake, Rais William Ruto amesema mazungumzo hayo yatafanyika kwa kuzingatia sheria na kuwa "upinzani ustarajie kupewa nyadhifa serikalini."
Vyama vyote vinaonekana kukubaliana katika masuala mengi, isipokuwa kuhusu gharama kubwa ya maisha na ukaguzi wa matokeo ya Uchaguzi wa Rais wa 2022 ambayo yanasisitiza kutatuliwa.
Kikao cha kwanza kinatarajiwa kufanyika siku ya Jumatano katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi.
Mchakato wa maridhiano kati ya Rais Ruto na Odinga uliafikiwa kufuatia mkutano wa faragha chini ya upatanishi wa aliyekuwa rais wa Nigeria, Ousegun Obasanjo.
Imetayarishwa na Shisia Wasilwa, DW Nairobi