Kambi za kisiasa Kenya kuchuana kuwania uspika
7 Septemba 2022Harakati za kuunda serikali mpya zimeanza rasmi. Kambi za Azimio la Umoja One Kenya na Kenya Kwanza zimewasilisha majina ya wagombea wa nafasi za spika wa bunge la taifa na baraza la Senate watakaochaguliwa kesho.Viongozi wote wataapishwa kesho Alhamisi ili kuanza kazi rasmi.
Kwa upande mwingine rais Uhuru Kenyatta amesisitiza tena kuwa atamkabidhi rais mteule madaraka bila shida ila anamtambua Raila Odinga kama kiongozi wake.
Duru zinaeleza kuwa kiongozi wachama cha Wiper Demokratic Kalonzo Musyoka ambacho ni mshirika muhimu wa Azimio la Umoja One Kenya ndiye atakewania nafasi ya spika wa baraza la Senate hata baada ya pingamizi za awali.
Viongozi wa Azimio wamekutana kwenye hoteli ya kifahari ya Masai Lodge iliyoko kaunti jirani ya Kajiado na kumpa ridhaa Kalonzo Musyoka kuwania nafasi hiyo.
Soma pia:Mahakama ya juu Kenya yaidhinisha ushindi wa Ruto
Kikao hicho kiliwaleta pamoja pia kiongozi wa NARC Kenya Martha Karua na rais anayeondka madarakani Uhuru Kenyatta.
Tim Wanyonyi ni mbunge mteule wa Westlands katika kaunti ya Nairobi na alikuwako kikaoni na ameiambia DW kwamba mkutano huo ni wa kawaida kuelekea mchakato wa kumpata ataewakilisha muungano huo kwenye mtifuano wa kumpata spika.
"Mtu mwenye umaarufu wake anaweza kupata kura hata kutoka upande mwingine." Alisema mbunge huyo mteule. Azimio:Wamchagua Madzayo kuwaniaunaibu spika wa Seneti
Mkutano huo wa Azimio kadhalika umeridhia kumuunga mkono seneta wa Kilifi Stewart Madzayo kuwa naibu spika wa Senate ambaye atachuana na mwenzake wa Meru,Kathure Murungi aliyependekezwa na Kenya Kwanza.
Wakati huohuo,muungano wa rais mteule William Ruto umempigia upatu gavana wa Kilifi wa zamani Amason Kingi kuwania nafasi hiyohiyo ya spika wa baraza la Senate.
Ifahamike kuwa mgombea wa ugavanawa kaunti ya Mombasa kwa tiketi ya UDA aliyeshindwa Hassan Omar alitupilia mbali azma ya kuwania uspika wa Senate baada ya mashauriano na rais mteule William Ruto na viongozi wengine wa Kenya Kwanza.
Spika mpya wa baraza la Senate atamrithi Kenneth Lusaka ambaye ni gavana mpya wa kaunti ya Bungoma.
Soma pia:Raila awasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa Ruto
Kuhusu uteuzi wa spika wa bunge la taifa,Azimio la Umoja One Kenya imemchagua spika wa zamani Kenneth Marende atakayemenyana na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula wa upande wa Kenya Kwanza.
Duru zinaeleza kuwa wagombea 9 kati ya wote 40 walioonyesha nia ya kuwania nafasi ya spika wa senate walikuwa wamerejesha fomu zao ilipofika saa nane unusu ambayo ni muda wa mwisho uliowekwa.
Bunge la 13 linakutana kwa mara ya kwanza kesho Alhamisi baada ya rais Uhuru Kenyatta kutangaza kikao rasmi cha pamoja na baraza la Senate kwenye gazeti la serikali.
Wabunge wa taifa na maseneta wataapishwa rasmi kwanza kabla ya kuwapigia kurawagombea wa spika wa Senate na bunge la taifa.Jeremiah Nyegenye ni karani wa baraza la Senate na anaelezea utaratibu wa kumchagua spika.
Wagombea hao wa nafasi ya spika kadhalika wanahitaji saini za wabunge rasmi 20 kutimiza vigezo vya ushindi.
Katika hatua nyingine,Rais Uhuru Kenyatta anayeondoka madarakani ameweka bayana kuwa atamkabidhi William Ruto madaraka aliyeshinda uchaguzi wa Agosti 9 ila anamtambua Raila Odinga wa azimio kama kiongozi wake.
Kufikia sasa bado Uhuru Kenyatta hajampongeza rais mteule hadharani.Kupitia mtandao wa Twitter,Duru zinaashiria kuwa William Ruto alimpigia siku mtangulizi wake ila upande wa pili haujathibitisha hilo kutokea.