Matumaini ni hafifu kuhusu usitishwaji mapigano huko Gaza
5 Mei 2024Matarajio ya kufikiwa kwa makubaliano ya usitishwaji mapigano katika vita vya Gaza yameonekana kuwa hafifu wakati wa mazungumzo mengine ya upatanishi mjini Cairo nchini Misri.
Kundi la Hamas limekataa makubaliano yoyote ambayo hayatohusisha kumalizika kabisa kwa vita na wanajeshi wa Israel kuondoka katika ardhi ya Palestina. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kamwe hawatokubaliana na matakwa hayo.
Wapatanishi kutoka Qatar, Misri na Marekani wanadhamiria kufikia makubaliano yatakayo vimaliza vita hivyo vilivyodumu kwa miezi saba, na wamependekeza kusitishwa kwa mapigano kwa muda wa siku 40 na kubadilishana mateka pamoja na wafungwa wa Kipalestina.
Soma pia: Misri ina matumaini kuwa Israel, Hamas watafikia makubaliano
Pande zote mbili wametupiana lawama kwa kukwamisha mazungumzo hayo huku Kiongozi Mkuu wa Kundi la Hamas Ismail Haniyeh akimtuhumu Netanyahu kwa kuhujumu juhudi za wapatanishi.