Mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza 'yafika pazuri'
14 Februari 2024Chanzo kimoja kutoka kundi la Hamas kililiambia shirika la habari la AFP kwamba ujumbe wa kundi hilo ulikuwa unaelekea kwenye mji mkuu huo wa Misri kukutana na wapatanishi wa nchi hiyo na wale wa Qatar, siku moja baada ya ujumbe wa Israel kufanya mazungumzo na wapatanishi.
Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki, ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa matendo ya Israel dhidi ya Gaza, naye pia alitarajiwa kuwasili Kairo kuzungumza na Rais Abdel Fattah al-Sissi juu ya suala hilo hilo.
Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), William Burns, alishiriki kwenye majadiliano ya jana Jumanne, yaliyomshirikisha pia mkuu wa Shirika la Ujasusi la Israel, Mossad.
Soma zaidi: Guterres atoa rai ya kusitishwa mapigano kuruhusu misaada Ukanda wa Gaza
Vyombo vya habari vya Misri viliripoti kwamba mazungumzo hayo ya jana kwa kiasi kikubwa yalikuwa "mazuri".
Msemaji wa Baraza la Usalama la Marekani, John Kirby, aliyaelezea majadiliano hayo kuwa ya "kujenga na yanayoelekea njia sahihi".
Wapatanishi wanaharakisha kupata makubaliano ya kusitisha mapigano kabla ya Israel kuendelea na uvamizi kamili wa ardhini kwenye mji wa kusini mwa Gaza, Rafah, ambako zaidi ya Wapalestina milioni 1.4 wamekwama.
Uwezekano wa mauaji ya maangamizi
Uwezekano wa mauaji ya watu wengi kwa pamoja umepelekea kauli kali kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni, hata kwa washirika wa karibu wa Israel, kuitaka serikali mjini Tel Aviv kutokutuma wanajeshi wake kwenye sehemu hiyo ya mwisho kabisa ambako raia wamekusanyika, baada ya kukimbia maeneo mengine ya Ukanda huo.
Marekani, ambayo ni mshirika muhimu wa serikali ya Israel, imesema haitaunga mkono operesheni yoyote ya wanajeshi wa ardhini huko Rafah, bila ya kuwapo kile inachokiita "mpango madhubuti" wa kuwalinda raia.
Soma zaidi: Israel na Misri zaruhusu misaada ya kibinaadamu kupelekwa Gaza
Rafah ndilo lango kuu la kupitishia misaada ya kibinaadamu na mashirika ya Umoja wa Mataifa yameonya kuwa kutatokea janga kubwa endapo mashambulizi hayo yataendelea.
Mkuu wa Huduma za Kiutu wa Umoja wa Mataifa, Martin Griffiths, alisema operesheni yoyote ya kijeshi itakuwa "mauaji makubwa ya kiholela."
Raia wenye khofu wanaripotiwa kujifungia kwenye majengo na mahema yao wakihaha kusaka njia ya kujinusuru na mauaji yanayowaandama.
Shinikizo la kuitaka Misri kuufungua mpaka huo kwa raia wa Kipalestina linaongezeka wakati huu wengi wao wakikabiliwa na mripuko wa homa ya ini na kipindupindu na uhaba wa maji salama na chakula.
Mmoja wao, Dana Abu Shaaban, akiwa kwenye mji huo wa mpakani na Misri anaotarajia ataruhusiwa kuuvuka akiwa na wanawe majeruhi, aliliambia shirika la habari la AFP: "Watoto wangu watatu wamejeruhiwa, nitakwenda wapi?"
Vyanzo: dpa, AFP