UNDP: Burundi inahitaji misaada zaidi ya kiutu
21 Februari 2018Kulingana na Garry Conille, muakilishi wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa nchini Burundi (UNDP), mahitajhi ya watu wa Burundi yamesababishwa na hali ya kijamii na kiuchumi na hata kuongezeka kwa majanga ya asilia.
Conille ameongeza kuwa matatizo kama haya yamesababisha hali ya maisha kuwa mbaya zaidi, kufikia huduma za msingi kuwa tatizo na pia kusababisha idadi kubwa ya watu kukosa makaazi yao.
"Tathmini ya mahitaji ya misaada ya kiutu ya taifa la Burundi inaonesha kuwa watu milioni 3.6 ambao ni thuluthi moja ya idadi jumla ya watu nchini humo watahitaji msaada huo mwaka huu, hali inayoashiria ongezeko la asilimia 20 ikilinganishwa na mwaka jana," alisema Conille.
Ameongeza kwamba wanawake na watoto ndio wanaoathirika haraka, huku utapia mlo ukisambaa kwa watoto waliyo chini ya miaka mitano katika mikoa minane kati ya mikoa 18 iliyoko Burundi.
Garry Conille, aliyasema hayo wakati alipokuwa anawasilisha mpango ulioandaliwa na taasisi ya misaada inayofanya kazi pamoja na serikali ya Burundi ambayo kwa kawaida inakataa kujihusisha na mipango kama hiyo inayofanywa na jamii ya Kimataifa.
Kwa mujibu wa makadirio ya UNDP serikali hiyo itapokea dola milioni 141 sawa na Yuro milioni 115 kushughulikia mahitaji hayo mwaka huu. Hata hivyo serikali haikukubali dondoo ya aina yoyote ya wapinzani kutajwa katika utafiti huo wa mahitaji ya misaada ya kiutu kwa taifa hilo la maziwa makuu.
Huenda kura ya maoni ya mwaka 2020 ikatoa nafasi kwa Nkurunziza kuongoza hadi 2034
Burundi iliingia katika mgogoro wa kisiasa mwaka 2015 wakati rais Pierre Nkurunziza alipotangaza kugombea muhula wa tatu madarakani licha ya ukomo uliyowekwa kikatiba ya mihula ya rais kuwa miwili pekee ya miaka mitano kila mhula.
Pierre Nkurunziza ambaye ni muasi wa zamanimwenye umri wa miaka 54 ameiongoza Burundi iliyo na idadi ndogo ya watu kwa miaka 12.
Wakosoaji wanamtuhumu kuwa dikteta anayekataa kuondoka madarakani. Kwa sasa serikali ya Burundi inapanga kuitisha kura ya maoni iliyo na utata inayotarajiwa kufanyika mwaka 2020 inayoweza kutoa nafasi kwa rais Nkurunziza kubakia madarakani hadi mwaka 2034.
Ghasia zilizotokea nchini humo mwaka 2015 zilisababisha vifo vya watu 1,200 huku zaidi ya watu 400,000 wakiachwa bila makaazi hii ikiwa ni kwa mujibu wa idadi zilizotolewa na mahakama ya kimataifa ya makossa ya uhalifu ICC.
Burundi iliyoorodheshwa kama moja ya mataifa masikini kabisa duniani, inakosa fedha za kigeni, mafuta ya petroli pamoja na kuwa na huduma mbaya za kiafya na ukosefu mkubwa wa chakula.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu