Mgogoro watokota kati ya India na Pakistan
27 Februari 2019Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa jeshi la Pakistan marubani wawili wa India walitekwa. Kuzidi kwa uhasama baina ya mataifa hayo mawili yanayomiliki silaha za nyuklia kulitokea muda mfupi baada ya
Pakistan kusema kuwa India ilifanya mashambulio ya mizinga na kuwaua raia sita kwenye mpaka unaolitenganisha jimbo la utatanishi la Kashmir. Kwa mujibu wa msemaji huyo raia wengine kadhaa walijeruhiwa katika mashambulio hayo.
Msemaji wa jeshi la Pakistan Meja jenerali Ghafoor pia amefahamisha kwamba moja ya ndege za India iliyoangushwa na majeshi ya Pakistan iliangukia katika ardhi ya Pakistan na nyingine iliangukia katika upande wa Kashmir unaodhibitiwa na India.
Wizara ya mambo ya nje ya Pakistan imesema ndege za jeshi la nchi hiyo zimefanya mashambulio kutokea ndani ya anga ya Pakistan na kwamba mashambulio hayo siyo ya kulipiza kisasi kutokana na ilichokiita ushari wa India unaoendelea. Wizara hiyo imesisittiza katika tamko lake kwamba mashambulio yaliyofanywa leo na ndege za Pakistan yaliepuka kusababisha vifo vya raia.
Waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan anatarajiwa kuitisha kikao cha mamlaka ya kitaifa inayosimamia silaha za nyuklia ili kujadili jinsi ya kujibu mashambulio yanayoafanywa na ndege za India.China imezitaka India na Pakistan kujizuia kuingia katika mgogoro zaidi. Marekani pia imetoa wito sawa na wa China wa kuzitaka pande zote mbili zijizuie. Wakati huo huo India imevifunga viwanja vyake vinne vya ndege kutokana na wasiwasi wa usalama. Maeneo ya mipakani yamewekwa katika hali ya tahadhari.
Waziri wa mambo ya nje wa Pakistan Shah Mahmood Qureshi amesema anawasiliana na mawaziri wenzake duniani kote kujadili alichoita uchokozi wa India. Waziri huyo amesema India inahatarisha amani katika eneo lao kwa kufanya mashambulio ya ndege dhidi ya Pakistan.
Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa India Sushma Swaraj amesema nchi yake haitaki kuendelea kwa mgogoro na Pakistan na kwamba itaendelea kuchukua hatua za busara na kujizuia. Waziri Swaraj ameeleza kuwa mashambulio yaliyofanywa na ndege za nchi yake kwenye kambi ya mafunzo ya magaidi ndani ya Pakistan yalikuwa na lengo la kuchukua hatua kali ili kuiteketeza miundombinu ya kigaidi ya kundi la Jaish-e-Mohammad.
Vyanzo: /AP/DPA/AFP