1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MichezoUfaransa

Michezo ya Olimpiki kwa walemavu yakamilika mjini Paris

9 Septemba 2024

Michezo ya Olimpiki kwa wanariadha wanaoishi na ulemavu imekamilika rasmi jana Jumapili katika mji mkuu wa Ufaransa Paris baada ya kudumu kwa siku kumi na moja.

https://p.dw.com/p/4kQm7
Paralympics | Schwimmerin Ali Truwit
Olimpiki| Paris| Muogeleaji Ali TruwitPicha: Julia Nikhinson/AP Photo/picture alliance

Wasanii mbalimbali walitumbuiza maelfu ya mashabiki katika uwanja wa Stade de France mbele ya wanariadha 4,400 kutoka mataifa 168 duniani kote.

Mratibu mkuu wa michezo hiyo Tony Estanguet amesema michezo hiyo ya Olimpiki imeandika kile alichokiita "majira ya joto ya kihistoria."

Estanguet, ambaye ni muendesha mashua wa zamani wa Olimpiki ameongeza kuwa, "Ufaransa ilikuwa na miadi na historia na kwamba michezo ya mwaka huu itasalia kwenye kumbukumbu za watu kwa muda mrefu.”

Amesema, "Rekodi nyingi za michezo zimevunjwa, na leo napendekeza tuvunje rekodi nyingine moja ili kuwaonyesha wanamichezo hawa mahiri jinsi walivyotupa msukumo wa kujiimarisha zaidi. Nawaomba nyote musimame ikiwa mutaweza, kuwapigia makofi, shangwe na vigelegele ambavyo hawajawahi kuviona maishani mwao."

Soma pia: Mwanariadha wa olimpiki wa Uganda afariki baada ya shambulizi la moto

Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Michezo ya Olimpiki kwa wanariadha walemavu Andrew Parsons ameisifu Ufaransa kwa kuweka mfano bora wa kuigwa kwa michezo ya siku zijazo.

China ilimaliza ya kwanza kwenye msimamo wa nishani kwa kuzoa medali 220 kwa ujumla: dhahabu 94, fedha 76 na shaba 50 huku Uingereza ikikamata nafasi ya pili kwa kushinda dhahabu 49, fedha 44 na shaba 31 wakati Marekani ikiridhika katika nafasi ya tatu kwa kushinda dhahabu 36, fedha 42 na shaba 27.

Ujerumani ilishikilia nafasi ya 11 kwa kushinda medali 49 kwa ujumla, 10 za dhahabu, 14 za fedha na 25 za shaba.