1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mji mkuu wa Ukraine, Kiyv watikiswa kwa mashambulio makali

29 Aprili 2022

Mji mkuu wa Ukraine umetikiswa kutokana na mashambulio makali yaliyofanywa na majeshi ya Urusi wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akifanya ziara nchini humo.

https://p.dw.com/p/4Aavf
Ukraine | Rauchwolken in Kiew nach Explosionen
Picha: John Moore/Getty Images

Kwa mujibu wa taarifa sehemu kadhaa zimepigwa katika mji mkuu, Kiyv kwa mara ya kwanza tangu majeshi ya Urusi yalipoondoka kwenye mji huo wiki zilizopita. Maafisa wanaoshughulikia mambo ya uokozi wamesema watu kadhaa wamejeruhiwa na wengine wamenaswa chini ya vifusi baada ya majengo mawili kuteketezwa.

Mashambulio hayo yalifanyika muda wa takriban saa moja baada ya Rais Zelensky na mgeni wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuzungumza na wandishi wa habari mjini Kiev. Guterres amesema Ukraine imegeuka kuwa kitovu cha maafa yasiyovumilika na ya kuumiza roho. Msemaji wa Katibu Mkuu huyo ameeleza kuwa Guterres yupo katika hali salama pamoja na ujumbe wake wote.

Kushoto: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. Kulia: Rais wa Ukraine Volodmyr Zelensky.
Kushoto: Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. Kulia: Rais wa Ukraine Volodmyr Zelensky.Picha: Efrem Lukatsky/AP/picture alliance

Wakati huo huo milipuko ilisikika nchini Ukraine kote ikiwa ni pamoja na mji wa Polonne uliopo magharibi na kwenye mji wa Chernihiv uliopo karibu na mpaka wa Belarus. Majeshi ya Urusi pia yamefanya hujuma kwenye mji wa Fastiv ambao ni kituo kikuu cha usafiri wa reli. Hata hivyo meya ya mji wa Odesa amesema makombora ya Urusi yalizuiwa angani.

Soma:Urusi yazikatia gesi Poland, Bulgaria, EU yasema imejipanga

Katika kadhia nyingine idara husika za serikali ya Ukraine zimesema Urusi ilifanya mashambulio makali kwenye jimbo la Donbas. Jimbo hilo la mashariki ndio makao makuu ya viwanda kwenye sehemu hiyo. Urusi imesema lengo lake kuu ni kuliteka jimbo hilo. Katika mji wa Mariupol wa kusini mwa Ukraine, wanajeshi wa nchi hiyo waliojibanza ndani ya kiwanda cha chuma bado wanaendelea kupambana. Kwa mujibu wa taarifa watu kadhaa waliuawa na wengine walijeruhiwa. Pana hofu ya kuzuka maradhi ya kuambukiza, kama kipindupindu katika mji huo kutokana na ukosefu wa maji safi. Mji wa Zaporizhzhia mwenye umri wa miaka 11 ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa.

Na wakati huo huo Rais wa Ukraine Volodmyr Zelensky ameishukuru Marekani kwa msaada wa fedha na amesema kuwa msaada huo ni hatua muhimu. Marekani inakusudia kutoa msaada wa dola bilioni 33 kwa Ukraine. Rais Joe Biden amewasilisha maombi ya msaada huo kwenye bunge la Marekani. Katika fungu hilo la fedha dola bilioni 20 zinakusudiwa kwa ajili ya ulinzi na dola bilioni 8.5 kwa ajili ya shughuli za kiuchumi.

Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Vladimir Astapkovich/TASS/Pool/dpa/picture alliance

Urusi kwa upande wake imeanza tena kupeleka gesi nchini Poland. Kampuni ya gesi ya Urusi Gazprom iliifungia Poland gesi baada ya kukataa kulipa kwa sarafu ya Urusi ya Rouble. Urusi pia imetishia kusimamisha ugavi wa gesi kwa nchi nyingine ikiwa zitakataa kulipa kwa sarafu ya Urusi, hatua inayozingatiwa kuwa ni ya kulipiza kisasi kutokana na vikwazo viliyvowekwa na nchi za magharibi dhidi ya Urusi.

Vyanzo: RTRE/DPA/AP