Misri imeahidi "mshikamano na huruma" kwa Syria
27 Februari 2023Ziara ya kwanza ya mwanadiplomasia mkuu wa Misri nchini Syria tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2011, katika ishara nyengine ya kuimarika kwa mahusiano kati ya Assad na mataifa ya kiarabu ambayo awali yalimtenga.
Ziara hii ni mfano wa karibuni zaidi wa mataifa ya kikanda kuonyesha maridhiano kwa serikali ya Rais Bashar al-Assad iliyotengwa kimataifa na kufukuzwa kutoka Jumuiya ya mataifa ya Kiarabu yenye makao yake mjini Cairo, baada ya mzozo wa Syria kuzuka mwaka 2011.
SOMA PIA; Syria yagubika mkutano wa Jumuiya ya Kiarabu
Shoukry anakuwa waziri wa tatu wa mambo ya nje wa nchi za Kiarabu kukutana na Assad tangu tetemeko la ardhi la Februari 6 lililoikumba Syria na nchi jirani ya Uturuki na kuwaua zaidi ya watu 50,000, baada ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Jordan kutuma wanadiplomasia wao wakuu.
Madhumuni ya ziara hii
Akizungumza na rais Assad pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Syria Faisal Mekded, Shoukry amesema amewasilisha ujumbe wa "mshikamano na huruma" kwa niaba ya Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi.
"Mahusiano kati ya mataifa haya mawili yameimarishwa vyema na yana nguvu. Daima tunafanya kazi kwa mshikamano na kukabiliana na changamoto zinazowakabili watu wa Syria, na tunatazamia Syria kuondokana na matokeo ya tetemeko hili la ardhi." Alisema Shoukry.
Rais Bashar al-Assad ameishukuru Misri kwa msaada wake wa kuunga mkono juhudi za serikali ya Syria kutoa misaada kwa walioathiriwa na tetemeko la ardhi. Misri ilituma ndege tatu na boti mbili zilizosheheni misaada ya kibinadamu.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kama uhusiano wa Misri na Syria utarejeshwa kikamilifu, Shoukry alisema kwamba madhumuni ya ziara yake ni ya "kibinadamu". Waziri huyo pia anatazamiwa kuzuru Uturuki, ambayo Cairo pia imekuwa na uhusiano mbaya nayo kwa muongo mmoja.
SOMA PIA; Muafaka wa Uturuki na Falme za Kiarabu watuliza mizozo
Hata hivyo mataifa kadhaa ya Kiarabu, kutoka Umoja Falme za Kiarabu, yamebadilisha mbinu kuelekea kurejesha uhusiano wao katika miaka ya hivi karibuni, baada ya Assad kuwashinda maadui zake katika sehemu kubwa ya nchi akisaidiwa na Iran na Urusi.
Washington imepinga hatua zozote za kusawazisha uhusiano na Assad, ikitolea mfano ukatili wa serikali ya Syria wakati wa vita na kueleza haja ya kuona maendeleo katika kupatikana kwa suluhu ya kisiasa.
Saudi Arabia, ambayo inasalia katika msuguano na Syria imesema makubaliano yanaundwa katika ulimwengu wa Kiarabu, na kuitenga Syria hakukuleta suluhisho na badala yake wanahitaji mazungumzo na Damascus katika kushughulikia masuala ya haki za kibinadamu.
/AFP