1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vikosi vya Assad vyaikamata Idlib

14 Machi 2012

Huku Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Kiarabu kwa Syria, Kofi Annan, akipokea majibu ya Rais Bashar al-Assad, vikosi vya serikali vimelichukua jimbo la Idlib kutoka upinzani baada ya mapigano makali.

https://p.dw.com/p/14KIk
Vikosi vya upinzani vyashindwa na vya serikali ya Syria katika jimbo la Idlib.
Vikosi vya upinzani vyashindwa na vya serikali ya Syria katika jimbo la Idlib.Picha: dapd

Baada ya mapigano makali ya siku nne, hatimaye vikosi vinavyomtii Rais Assad ndivyo vinavyolidhibiti jimbo la kaskazini la Idilib, kwa mujibu wa wanaharakati wa upinzani. Rami Idlibi, mmoja wa wanaharakati hao, ameliambia shirika la habari la Ujerumani (DPA) kwamba wapiganaji wao walishambuliwa vibaya sana na vikosi vya serikali na hivyo kujiondoa kabisa kwenye eneo hilo.

Ingawa hadi sasa hakujawa na ripoti zinazotaja idadi kamili ya watu waliouawa na au kujeruhiwa, lakini shirika la habari la AFP limethibitishiwa na watu walioko ndani ya jimbo hilo, kwamba operesheni ya kijeshi ya vikosi vya serikali imekuwa kubwa sana. Mmoja wa wakaazi wa huko, Noureddin al-Abdu ameiambia AFP kwamba mapigano kwa sasa yamesita na kinachoendelea ni msako wa nyumba kwa nyumba unaofanywa na vikosi vya serikali.

Kutekwa kwa mji wa Idilib na vikosi vya Rais Assad kumekuja wiki mbili baada ya vikosi hivyo kuushambulia na kuutia mikononi mji mwengine wa Bab Amr, ambao ni kitovu cha ngome ya upinzani kwenye jimbo la Homs, ambako nako kulisababisha mamia ya watu kuuawa.

Annan apokea majibu ya Assad

Wakati hayo yakiendelea, msemaji wa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Kiarabu kwa Syria, Kofi Annan, amesema kwamba Rais Assad amemtumia majibu rasmi mjumbe huyo. Annan aliitembelea Syria mwishoni mwa wiki iliyopita na kumpa Rais Assad kile alichokiita "mpango madhubuti" wa kuleta amani.

Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Koffi Annan (kushoto) akizungumza na Rais Bashar al-Assad wa Syria.
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, Koffi Annan (kushoto) akizungumza na Rais Bashar al-Assad wa Syria.Picha: picture-alliance/dpa

"Bwana Annan amepokea jawabu kuroka kwa Rais Asad. Baadaye leo atakuwa na mengi ya kuelezea kutokana na jawabu hilo." Amesema msemaji wa Annan, Ahmad Fawzi. Bado haijuilikani kilichomo kwenye majibu hayo, lakini inatarajiwa kwamba ni mtiririko wa ahadi za Rais Assad kusitisha mapigano na kuleta mageuzi.

Hapo jana Bunge la Syria lilisema kwamba Rais Assad ameamuru uchaguzi wa bunge kufanyika tarehe 7 Mei. Uchaguzi huo utafanyika chini ya katiba mpya iliyopitishwa kwa kura ya maoni mwezi uliopita, ambayo upinzani na nchi za Magharibi na waungaji mkono wao wa Kiarabu, waliita ni aibu.

Jumuiya ya Kimataifa haijafanya ya kutosha

Hadi sasa hakujakuwa na hatua ya pamoja kutoka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya serikali ya Syria, huku Urusi na China ambazo ni wanachama wa kudumu wa Baraza hilo zikiunga mkono ahadi za mageuzi za Rais Assad na kuzuiwa kila jaribio la kumbana kiongozi huyo kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao.
Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao.Picha: AP

Hata hivyo, hivi leo (14.03.2012) Waziri Mkuu wa China, Wen Jiabao, alisema kwamba nchi yake haipendelei upande wowote katika mgogoro wa Syria, na kwamba inaumizwa sana mateso yanayowapata Wasyria. Mapema, vyombo vya habari vya serikali ya China vilisema kuwa serikali ingelitoa msaada wa dola milioni mbili za Kimarekani kama msaada wa kibinaadamu kwa watu wa Syria kupitia Shirika la Msalaba Mwekundu.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, alisema hapo jana kwamba vikosi vya Syria havitaacha kupambana au kujiondoa katika maeneo vinavyoyashikilia hadi hapo vikosi vya waasi vitakapodhibitiwa.

Umoja wa Mataifa unasema hadi sasa watu 8,000 wameshauwa nchini Syria huku Wasyria 230,000 wakiwa wameyakimbia makaazi yao tangu maandamano dhidi ya serikali yaanze miezi kumi na mbili iliyopita.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPAE/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman