Misri na timu nyingine tano zatinga 16 bora ya AFCON
20 Januari 2022Ulikuwa ni mpira wa kona uliomaliziwa na kichwa kikali kilichopigwa na mshambuliaji wa Misri Mohamed Abdelmonem ndiyo uliiwezesha timu hiyo kuwakalisha chini mahasimu zao Sudan dakika 10 tu kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika.
Ushindi huo wa Misri umefungua njia kwa timu nyingine tano kujiunga kwenye hatua ya mtoano ikiwemo Ivory Coast. Nyingine ni Mali, Gambia, Malawi na Cape Verde. Nigeria iliyo pia kwenye kundi D ilijipatia ushindi wa tatu mfulilzo jana Jumatano kwa kuilambisha kibuyu cha asali Guinea Bissau cha bao 2-0.
Ushindi huo umeifanya Nigeria kuwa kileleni mwa kundi D na Misri kuwa nafasi ya pili, msimamo utawalazimisha mafarao hao kukwaana na washindi wa kundi E katika hatua ya mtoano. Na wengi wanatabiri itakuwa ni kati ya Misri na Ivory Coast.
"Nadhani Misri ilistahili kushinda mchezo huu bila wasiwasi wowote ukitilia maanani nafasi tulizojitengenezea na kambumbu tulilosakata" amesema Carlos Queiroz, kocha wa timu ya taifa ya Misri, ambayo ni washindi mara saba wa michuano ya kandanda barani Afrika, AFCON.
Matamshi ya kocha huyo yanasadifu ukweli uliodhihirika uwanjani. Misri ilionekana wazi kuizidi nguvu Sudan na walipata nafasi chungu nzima za kuoneza goli jingine lamini hilo halikufanikiwa.
Sudan yaaga mashindano huku Nigeria ikiendeleza ubabe
Kipigo walichoambulia Sudan ndiyo ilikuwa tikiti ya wao kukasanya virago na kuyaaga mashindano ya AFCON.
Ushindi wa Misri ndiyo uliihakikishia timu ya taifa ya visiwa vya Cape Verde na ile ya Malawi nafasi ya kusonga mbele kupitia dirisha la timu zilizofanya vizuri zaidi kwenye nafasi ya tatu ya makundi.
Ivory Coast inaongoza kundi E ikiwa na alama 4 na hakuna uwezekano kuwa itashindwa kufuzu hatua ya 16 bora.
Hilo pia limeonekana kwa timu za Mali na Gambia za kundi F ambazo zote tayari zina pointi 4 kila moja baada ya michezo miwili.
Katika mchezo kati ya Nigeria na Guinea Bissau, Nigeria iliendeleza ubabe wake tangu kuanza michuano hiyo kwa kupachika wavuni mabao mawili wakati wa kipindi cha pili yaliyfungwa na Umar Sadiq na nahodha wa timu hiyo William Troost-Ekong.
Kocha wa muda wa timu ya taifa ya Nigeria, ambayo imekwishawahi kutwaa kombe la AFCON mara tatu huko nyuma, alifanya mabadiliko mara nane kwenye mchezo wa jana Jumatano. Lakini ilikuwa ni mabadiliko yaliyomwingiza Kelechi Iheanacho ndiyo yalizaa matunda baada ya kupiga pasi safi iliyomaliziwa vizuri na Sadiq kwenye dakika ya 56 ya mchezo.
Picha kamili ya hatua ya mtoano yaanza kuonekana
Nigeria watasalia mjini Garoua kucheza na timu itakayomaliza nafasi ya tatu bora kwenye hatua ya mtoano siku ya Jumapili.
Cape Verde watakwaana na Senegal mjini Bafoussam mnamo Januari 25 wakati siku hiyo hiyo Malawi - iliyoingia kwa mara ya kwanza kwenye hatua ya mtoano wa mashindano ya AFCON - watakipiga na Morocco mjini Yaounde.
Michezo mingine ya hatua ya mtoano itafahamika baada ya duru ya mwisho ya michezo ya kundi E na F itakayochezwa leo Alhamisi.
Algeria inayotetea kombe na ambayo rikodi yake ya kutokufungwa kwenye mechi 35 ilikatizwa na Guinea ya Ikweta mapema wiki hii, italazimika kuidhibu Ivory Coast mjini Douala kuepuka fedheha ya kuambulia pointi moja tu katika michezo miwili iliyokwishacheza.
Guinea ya Ikweta iliyo nafasi ya pili kwenye kundi E itakabiliana na Sierra Leone ambayo ililazimisha sare ya bila kufungana kwenye mchezo wake wa ufunguzi na Algeria na kisha kupapatua sare nyingine ya bao 2-2 mbele ya Ivory Coast.
Michezo mingine ya leo itakuwa ni ya kundi F kati ya Tunisia na Gambia na ule kati ya Mali na Mauritania.