1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri, Ufaransa yataka misaada ifikishwe Gaza

17 Oktoba 2023

Serikali ya Misri na ile ya Ufaransa imetaka kuharakishwa kwa misaada ya kibinaadamu kuingia kwenye Ukanda wa Gaza wakati huu Israel ikiendeleza mashambulizi yake dhidi ya ukanda huo ulio sehemu ya Mamkala ya Palestina.

https://p.dw.com/p/4XaTi
Israel | Israelisches Militär mit Panzer
Kifaru cha jeshi la Israel kikisogea karibu na mpaka wa Gaza siku ya Jumapili (Oktoba 15).Picha: Ohad Zwigenberg/AP Photo/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Sameh Choukry, na mwenzake wa Ufaransa, Catherine Colona, wamehimiza kufikishwa kwa misaada ya kibinaadamu na kufanikisha zoezi la kuondoka kwa raia wa kigeni katika Ukanda wa Gaza unaoendelea kushambuliwa kwa mabomu na jeshi la Israel.

Kauli hiyo inakuja wakati Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesisitiza kuwa hakuna usitishwaji wowote wa mapigano na Hamas.

Soma zaidi: UN: Mzozo wa Israel na Hamas umefikia hatua mbaya

Umoja wa Mataifa umeonya mara kwa mara juu ya hali mbaya ya kibinadamu huko Gaza, baada ya Israel imetangaza "kuzingira kikamilifu" ukanda huo na hivyo kusitisha huduma muhimu kwa watu wapatao milioni 2.4 wanaoishi eneo hilo.

Misri inadhibiti kivuuko cha mpakani cha Rafah, ambayo ndio njia pekee ya kuingia na kutoka Gaza isiyodhibitiwa na vikosi vya Israel.

Vita vya Israel dhidi ya Ukanda huo vimeingia siku ya 10 na takribani watu 2,750 wameshauawa huko Gaza.

Israel ilitangaza vita dhidi ya kundi la Hamas, ambalo linachukuliwa kuwa la kigaidi na Umoja wa Ulaya na Marekani, baada ya kundi hilo kuvamia na kufanya mauaji ya watu 1,400 nchini Israel na kuwachukuwa wengine wapatao 200 kuwa mateka.