1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSomalia

Misri yasema haitaruhusu vitisho kwa Somalia au usalama wake

22 Januari 2024

Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi amesema nchi hiyo haitaruhusu vitisho vya aina yoyote kwa Somalia baada ya Ethiopia kusema itazingatia kuutambua uhuru wa Somaliland ili kupata fursa ya kuifikia Bahari ya Sham.

https://p.dw.com/p/4bWVM
Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi
Rais wa Misri Abdel Fattah El-SisiPicha: Jacquelyn Martin/Pool/AP Photo/picture alliance

Katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud aliyeitembelea Misri, al-Sisi amesema Misri haitaruhusu mtu yeyote kuitisha Somalia au kuathiri usalama wake.

Kauli hiyo ya al-Sisi ni ishara kwamba Misri inaweza kuhusika moja kwa moja katika mzozo huo ambao umeibua mvutano mpya katika eneo la Pembe ya Afrika. 

Somaliland ilijitangaza uhuru wake kutoka Somalia mwaka 1991 japo haijatambuliwa na nchi yoyote.

Uhusiano kati ya Misri na Ethiopia, ambazo zinatumia kwa pamoja mto Nile, umekuwa sio mzuri kwa muda mrefu kutokana na bwawa lililojengwa na Ethiopia katika mto wa Blue Nile.