1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaAfrika

Mkakati mkali wa Uganda wafanikiwa kudhibiti COVID

5 Agosti 2020

Uganda ilifunga shule, kusitisha mikusanyiko mikubwa kabla ya kisa cha kwanza. Imerikodi vifo vitano tangu Machi huku idadi ndogo ya visa ikitofautiana pakubwa na Afrika Kusini. Ni wakati Afrika ikikaribia visa milioni.

https://p.dw.com/p/3gS7t
Straßen von Kampala, der Hauptstadt von Uganda
Picha: picture-alliance/AA/A. Lubowa

Mfumo ulioporomoka wa hospitali za umma nchini Uganda, migomo ya madaktari na kashfa za rushwa vinayafanya mafanikio katika mapambano dhidi ya virusi vya corona kuwa jambo lisilowezekana.

Lakini taifa hilo la wakaazi milioni 42 limerikodi visa zaidi ya 1,200 tu na vifo vitano tangu mwezi Machi, idadi ndogo kabisaa kwa taifa kubwa kama hilo.

Wakati idadi ya visa barani Afrika ikikaribia milioni moja, uzoefu wa Uganda unaonyesha kile kinachoweza kufanikishwa pale serikali yenye udhibiti mkubwa wa madaraka inapochukuwa hatua haraka na kutekeleza marufuku kali ya kutotoka nje ovyo. Lakini mafanikio yake yanakuja kwa gharama, wanasema wakosoaji.

Ajira zilipotea, na ukuaji wa uchumi unatarajiwa kushuka kwa asilimia 0.4 mwaka 2020, kutoka asilimia 5.6 mwaka uliopita, kwa mujibu wa Benki ya Dunia.

Uganda  Kampala | Technikindustrie sucht man kreativen Mitteln Corona zu behandeln
Sekta ya teknolojia imekuwa ikibuni njia rahisi za kukabiliana na mripuko wa Covid-19, katika taifa amabalo mfumo wake wa afaya uko dhaifu sana.Picha: Prof. Vincent Sembetya

Baadhi ya wanawake wajawazito wamekufa wakijifungua, baada ya kushindwa kufika hospitali kwa sababu ya vizuwizi vya kusafiri. Vikosi vya usalama vinakosolewa na makundi ya haki za binadamu kwa ukiukaji - vipigo na ukamataji wa baadhi ya waliokiuka sheria.

Viongozi wa upinzani wanaituhumu serikali kwa kutumia janga hilo kama kisingizio cha kuzuwia mikusanyiko ya kisiasa na kuwakamata wapinzani, tuhuma ambazo serikali inakanusha.

"Mtu asie na kazi ni bora kuliko mtu aliekufa," naibu waziri wa afya Robinah Nabbanja aliliambia shirika la habari la Reuters. "Hatua za karantini ni halali kabisaa."

Usitishaji wa shughuli za maisha

Mkakati wa Uganda unatofautiana na mataifa mengi ya Afrika, ambayo hayakuweka hatua kali kama hizo na yalianza kulegeza hatua hizo kabla ya maambukizi kufikia kilele ili kulinda chumi zao dhaifu na raia ambao kwa asilimia kubwa ni masikini.

Baadhi yanakabiliwa na miripuko inayoongezeka kwa kasi na inayoweza kuielemea mifumo ya afya ya umma, limeonya shirika la afya duniani, WHO.

Hatua kali za Uganda ziliipa serikali muda wa kuuanda mfumo wake wa afya na kujifunza kuhusu ugonjwa huo, anasema Tim Bromfield, mkurugenzi wa ukanda wa Afrika na Kusini mwa Afrika, katika taasisi ya ushauri ya Tony Blair kwa ajili ya Mabadiliko Duniani yenye makao yake nchini Uingereza.

Coronavirus Uganda Kampala Temperaturmessung
Mfanyakazi wa kujitolea wa shirika la Msalaba Mwekundu akimpima mwanaume joto kabla ya kuingia katika soko la Nakasero mjini Kampala, Aprili 1, 2020.Picha: AFP/S. Sadurni

"Serikali zote zinaweka urari kati ya kulinda maisha na njia za kujipatia riziki."

Uganda ilifunga shule na kupiga marufuku mikusanyiko mikubwa siku tatu kabla ya kuthibitisha kisa cha kwanza Machi 21. Kufikia mwishoni mwa mwezi Machi, biashara nyingi zaidi zilikuwa zimefungwa, mzunguko wa magari kupigwa marufuku, na amri ya kutotembea usiku ikatekelezwa. Uvaaji wa barakoa ukawa wa laazima katika maeneo ya umma mnamo mwezi Mei.

Uitikiaji wa taifa hilo la Afrika Mashariki uliundwa na mapambano dhidi ya magonjwa hatari kama Ebola na virusi vya Marburg, wanasema wataalamu wa afya ya umma.

Unaweza kusoma pia Zaidi ya watu 800,000 wameambukizwa virusi vya corona barani Afrika

Taifa hilo lilikuwa tayari kwenye tahadhari kutokana na mripuko wa Ebola katika taifa jirani la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wakati COVID-19 iliposhambulia, alisema Alex Ario, mkurugenzi taasisi ya taifa ya afya ya umma, yenye mafungamano na serikali.

Timu ziliandaliwa kuielimisha umma na kuwafuatilia walioathiria. Abiria walikuwa tayari wanachunguzwa kwenye viwanja vya ndege. Wodi za kutengwa wagonjwa zilikuwa tayari kupokea wagonjwa, na yeyote alieathirika alilazwa hospitali.

"Uganda ilijua wapi pa kufanyia uchunguzi wao," alisema John Nkengasonga, mkuu wa vituo vya Afrika vya kupambana na kuzuwia magonjwa. "Somo kutoka kwao ni kwamba unapaswa kujua janga lako."

Uganda Johannesburg  Coronavirus Maßnahmen Polizei
Askari wa kikosi cha kijeshi cha Uganda, maarufu LDU, akimchapa fimbo mchuuzi mtaani kwa madai ya kukiuka kanuni za kudhibiti mripuko wa COVID-19.Picha: Getty Images/AFP/B. Katumba

Uganda - kama ilivyo China - inaweza kutekeleza hatua kali za udhibiti kukiwa na upinzani mdogo wa ndani.

Mnamo mwezi Machi, vyombo vya habari nchini humo vilichapisha picha za kundi lenye hadhi ya kijeshi wakiwapiga wauza matunda na wapita njia kwa kuvunja vikwazo vya kazi na usafiri. Msemaji wa jeshi Brigedia Flavia Byekwaso alisema "walipitiliza katika kusimamia utekelezaji wa hatua hizo."

Bruce Kirenga, anaeongoza taasisi ya mapafu ya chuo kikuu cha Makerere, alisema hatua thabiti za afya ya umma huenda zilipunguza kiwango cha virusi katika mzunguko.

Soma zaidi: Museveni atangaza mkakati kuokoa uchumi baada ya corona

Alibainisha kwamba karibu asilimia 95 ya visa vya Uganda ni vile visivyoonyesha dalila au vya dalili za wastani. Baadhi ya wanasayansi wanapendekeza kwamba wagonjwa walio na idadi kubwa wa vijidudu vyambukizavyo magonjwa ndiyo wanakuwa na visa vikali zaidi.

Njaa yakandamiza

Nchi jirani ya Rwanda, ambayo ilichukuwa pia mkakati mkali, imerikodi vifo vitano katika taifa la wakaazi milioni 12. Mataifa mengine yalio na idadi ndogo ya vifo ni pamoja na taifa dogo la kisiwa la Shelisheli, ambalo lilifunga haraka mipaka yake na halina vifo, pamoja na Botswana, yenye idadi ya wakaazi chini ya milioni 2.5 na vifo viwili.

Afrika Kusini iliweka mojawapo ya vizuwizi vikali zaidi duniani ilipokuwa na visa 400 tu. Lakini hatua hizo ziliuathiri uchumi wake uliokuwa tayari unadorora, na serikali ilianza kuelegeza baadhi ya hatua hizo ndani ya wiki chache, chini ya shinikizo kutoka kwa viongozi wa sekta ya biashara, vyama vya wafanyakazi na vyama vya upinzani.

Hivi sasa inakabiliwa na janga ambalo linachangia karibu nusu ya visa vya bara la Afrika vipatavyo 975,000 na vido 21,000.

Wataalamu wa afya ya umma wanaamini idadi ya maambukizi na vifo barani Afrika ni kubwa kuliko tarakimu rasmi zinavyoonyesha, wakibainisha viwango vidogo vya upimaji katika mataifa mengi. Lakini mbali ya machache tu, mataifa hayajaripoti matukio yoyote ya hospitali kuelemewa na wagonjwa.

Coronavirus Uganda Kampala Regierung verteilt Lebensmittel
Serikali ya Uganda iligawa chakula kwa baadhi ya maeneo ambayo yalitazamiwa kuathirika zaidi na hatua za kuzuwia kusambaa kwa virusi vya Corona. Lakini baadhi wanasema chakula hicho hakikuwafikia.Picha: Reuters/A. Lubowa

Tarakimu za Uganda zinachukuliwa kuwa za kuaminika kuliko mataifa mengi: Nchi hiyo imefanya vipimo zaidi ya 250,000 na inashirikiana kwa karibu na taasisi za kimataifa, alisema Dk. Peter Waiswa, mtaalamu wa afya ya umma katika taasisi ya sayansi ya afya ya chuo kikuu cha Makerere.

Soma zaidi Shughuli za kiuchumi zaanza kurejea nchini Uganda

Uganda hivi sasa inalegeza hatua zake za kusitisha shughuli, lakini watu kama Wilson Munyakayanza wanataka ziondolewe. Baba huyo wa watoto watatu hajafanya kazi tangu alipopoteza kazi yake kama meneja wa baa mwezi Machi.

"Nashinda njaa wakati mwingine na nakula moja tu kwa siku," alisema. Virusi vya corona siyo tu vimetuua lakini janga la kushinda na kulala njaa haliko mbali sana na kifo."

Chanzo: Reuters.